NEWS


NIHALI YA HATARI KATIYA TANZANIA NA MALAWI!!

SERIKALI ya Tanzania imeitaka Serikali ya Malawi kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa kuhusu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na kuyataka makampuni yanayoendelea kufanya utafiti katika ziwa hilo kuacha mara moja.
Msimamo wa Tanzania umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, zikiwa ni siku chache tangu Malawi kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, kutangaza kuwa Ziwa Nyasa ni mali yao kwa mujibu wa mkataba wa Heligoland uliowekwa saini Julai mosi mwaka 1890.
Tanzania imesema njia bora ya kumaliza tatizo la mpaka wa ziwa hilo ni kwa mazungumzo ya amani, na kwamba katika kipindi hicho Malawi isiruhusu mtu au kikundi chochote kufanya utafiti kwenye eneo linalobishaniwa.
Waziri Membe alifafanua kuwa, linapozungumziwa Ziwa Nyasa, wanazungumzia maisha ya wananchi 600,000 wanaoishi katika mwambao wa ziwa hilo, kwamba kwao ziwa hilo ni urithi wao, chanzo cha uzima na maendeleo. Kwa vyovyote serikali ina dhamana ya kuwalinda.
Hivyo Membe kwa niaba ya serikali aliyaonya makampuni yote yanayofanya utafiti kwenye eneo hilo kusitisha mara moja, kwamba Tanzania haitaruhusu utafiti huo kuendelea hadi makubaliano na majadiliano kuhusu mpaka yatakapofikiwa na pande hizo mbili.
Tanzania kwa upande wake imesema mpaka wa kweli kati yake na Malawi unapita katikati ya ziwa, hivyo kufanya eneo lote la kaskazini mashariki ya ziwa kati ya latitudo nyuzi 9 na 11 kuwa ni mali yake kwa mujibu wa mkataba huohuo wa Heligoland wa mwaka 1890.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema kuwa Tanzania iko tayari kwa uchokozi wa aina yoyote ile kwani ni nchi iliyosaini na kufuata mikataba ya kimataifa.
Tunaipongeza serikali yetu kwa kutaka kumaliza mgogoro huu kwa busara bila ya mataifa haya kuingia kwenye vita. Lakini pamoja na staha hiyo, Tanzania inapaswa kuchukua tahadhari kwani vita hii inayochochewa si baina yake na Malawi pekee.
Dunia nzima sasa inaelewa kuwa Tanzania imepata gesi na madini ya uranium katika maeneo mengi ya mikoa ya kusini, hatua inayoyafanya mataifa makubwa kuanza mbinu za kutaka kunufaika na rasilimali hizo ama kwa njia sahihi au zisizo sahihi.
Hivyo basi kwa maoni yetu, Serikali ya Malawi ni kama inatumiwa na mataifa makubwa yenye maslahi na gesi yetu ili kuzusha tafrani ya mipaka na tutakapoingia kwenye vita wao watasaidia silaha huku wakiendelea kujichotea rasilimali hiyo.
Tunasema hivyo kutokana na kushuhudia mifano hii kwenye mataifa ya jirani zetu kama Sudan na Sudan Kusini, DR Congo na Rwanda, Nigeria na mengineyo ambayo yanapigana huku mataifa makubwa yanayojifanya kuwasaidia yakiendelea kujichotea rasilimali ya mafuta.
Ni katika hatua kama hii, tunaitaka serikali yetu kuwa makini kwa kujiimarisha kijeshi mipakani licha ya kutaka jambo hili kumalizwa kwa busara kwani adui anayetuchokoza ana malengo na ajenda zaidi ya Ziwa Nyasa kama tunavyodhani.

No comments:

Post a Comment