LEO nilitaka kuwazawadia nafasi hii wasanii waliofanya vizuri katika sanaa Bongo lakini kwa bahati mbaya kuna jambo ambalo nikiliacha likavuka mwaka 2012 kwenda 2013, litasababisha majanga.
Ngoja tuangalie mwenendo mzima wa wasanii wetu wa filamu za Kibongo ambao tabia zao za kujiona wao ni wao na hakuna mtu anayeweza kuwapinga katika uamuzi wao zimekithiri.
Kikundi kidogo kilichoanzishwa miaka miwili iliyopita kinachojulikana kwa jina la Bongo Movie, kimekuwa kama kichaka cha kila uovu unaotajwa duniani. Wasanii wanaounda kikundi hicho wanajifanya wao ndiyo wafalme wa mbingu na nchi kutokana na maazimio ya ajabu ambayo wamekuwa wakijiwekea kwenye vikao vyao wanavyofanya usiku katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar vikidaiwa kuambatana na mambo ambayo nisingependa kuyazungumza hapa leo.
Hivi mwenyekiti wa Bongo Movie Unit, Vincent Kigosi ‘Ray’ na makamu wake, Irene Uwoya mnataka kuwapeleka wapi wasanii wa filamu ambao wako ndani ya kikundi chenu?
Mara nyingi nimepokea manung’uniko ya waigizaji kadhaa kuwa mmekuwa mkitawala kibabe kiasi kwamba mnawakataza wasanii wenu hao wasiwe na uhusiano mzuri na waigizaji wengine hata yanapotokea matatizo. Kuna ubaguzi wa hali ya juu.
Tukirudi nyuma, enzi za utawala wa mwenyekiti mstaafu, Steven Jacob ‘JB’ hakukuwa na mfumo kama huu mnaotumia. Imefika mahali sasa hivi hata wanachama wenu wakiugua hamtoi ushirikiano japo mkisikia kuna msiba ndiyo mnajiweka mstari wa mbele. Mnaonesha umaarufu, mnauza sura na mavazi mapya. Bila kusahau zile miwani kubwa nyeusi za jua!
Katika kudhihirisha kuwa ninyi viongozi mnatawala kibabe, hivi karibuni baada ya msanii mwenzenu ambaye anasumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ kuandaa tamasha mkoani Arusha kwa ajili ya kuchangisha fedha za matibabu India, mlikubaliana naye.
Cha ajabu siku chache kabla ya tamasha, mlibadili mawazo baada ya kupata dili la fedha mkoani humo na kwenda kufanyia sehemu ileile aliyokuwa ameandaa Sajuki kwa ajili ya tamasha lake, hali iliyosababisha afya yake kuyumba kwa mara nyingine hadi unapokodolea macho maandishi haya.
Kutokana na kuona aibu kwa kitendo hicho, habari za ndani zinadai kuwa mweka hazina wenu, Single Mtambalike ‘Richie Richie’ alimuahidi Sajuki kuwa mmekubaliana mtampa Sh. milioni tatu kutokana na usumbufu uliojitokeza lakini mpaka sasa hamjampa chochote. Mbaya zaidi kuna madai kuwa mmegoma kwenda kumjulia hali katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa.
Swali la kujiuliza ni je, klabu yenu hiyo ipo kwa ajili ya sherehe tu kama mlivyofanya kwenye pati ya Shamsa Ford au ni kwa ajili ya kusaidiana katika kila jambo?
Kwa jinsi mnavyoendesha mambo ni wazi kuwa mpo kwa ajili ya sherehe na kuonesha ufahari kwenye misiba, jambo ambalo linatia aibu. Kwani ninyi hamtakufa?
Ngoja nikukumbushe Uwoya, hivi karibuni ulifanya sherehe ya kuzaliwa. Mchana ulikwenda kutoa misaada kwa wagonjwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar. Ni jambo zuri. Watu tukajua mambo yamekwisha lakini giza lilipoingia tu, ukafanya pati inayodaiwa kugubikwa na vitendo ya ufuska huko Mbezi-Beach na kuwapiga marufuku waandishi wa habari wasifike kwenye sherehe yako.
Kwa habari zilizovuja kutoka huko ni kwamba wasanii wote waliohudhuria walipigwa marufuku kupiga picha kwani mlikuwa ndani ya mavazi ya kuogelea yaani wasichana walivaa vichupi huku wanaume wakiwa ndani ya boksa na singlendi. Hivi unajijua kuwa umeshuka sana kisanaa? Mwaka 2013 badilika, achana na tabia hizo.
Hivi Ray na Uwoya, mnadhani kwa kuliongoza kundi lenu kumkatili Sajuki anayehitaji msaada mtakuwa hamjatenda dhambi? Hakuna ufalme unaodumu milele isipokuwa wa Mungu tu. Jitambueni na mumuogope Mungu kwani malipo ni hapahapa duniani. For the love of game!
No comments:
Post a Comment