Tuesday, March 12, 2013

Lusifa Aliniita Kuzimu-23


Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale yule Mwarabu alipofika nyumbani kwa David akiwa na wenzake aliowaacha kwenye gari lake. Baada ya kuzungumza na kijana huyo aliwafuata, wakateremka garini ndipo akaanza kuwaonyesha eneo la David. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…
Waarabu hao walizungumza lugha yao ndipo yule mwenyeji akaniambia alikuja kama alivyokuwa ameahidi lakini pale nyumbani hapakuwa mahali pazuri kwa mazungumzo yetu.
Mwarabu huyo ambaye siku hiyo alivaa vizuri zaidi kuliko siku ya awali, aliniomba nipande kwenye gari ili twende sehemu iliyofaa kwa mazungumzo.
Aliponiambia hivyo niliogopa sana na kubaki nikijiuliza kama wakienda kunichinja huko na kunichuna ngozi itakuwaje, kwa ujumla nilipa hofu kwani niliwahi kusikia baadhi ya matajiri walikuwa na tabia ya kuua watu.
Nikiwa nawaza hivyo, yule Mwarabu aliniomba niingie kwenye gari kwani muda ulikuwa unakwenda ndipo nilimweleza ngoja nikafunge mlango.
Nilipoingia ndani nilitumia kama dakika tatu kufikiria kama niondoke nao au nisiondoke lakini baadaye nikapiga moyo konde na kusema Mungu angenilinda.
Baada ya kufunga milango nilitoka nikaingia kwenye gari, akaliondoa na kuanza kuelekea barabara ya kwenda mjini, kidogo mapigo ya moyo yalipoa.
Tulitumia kama dakika kumi tukawasili kwenye hoteli moja nzuri ya ghorofa, akaegesha gari tukashuka akatuambia tumfuate.
Tulimfuata hadi sehemu iliyokuwa na lifti tukaingia, akabonyeza kitufe tukapanda hadi ghorofa ya mwisho tukaingia kwenye sehemu iliyokuwa na meza kubwa na viti zaidi ya sita,Tv na vitu vingine.
 Tukiwa tumeketi, yule Mwarabu alimwita mhudumu ambaye alifika na kumsikiliza kila mmoja wetu alihitaji kula na kunywa nini!
Licha ya kunywa chai nyumbani, nilimwambia aniletee chai, chapati mbili na mayai mawili ya kukaangwa, wao wakaagiza soda.
Nikiwa nakunywa chai na wao wakiendelea kunywa vinywaji vyao, yule Mwarabu akaniambia kwamba jana nilimuuliza ili niwe tajiri natakiwa kufanya nini, nikawambia sawa kabisa nilitaka kujua jambo hilo.
Baada ya kumweleza hivyo, alicheka na kuniambia kama nilihitaji kuwa tajiri kwanza nipunguze matumizi yasiyo ya lazima na niache starehe kama kunywa pombe nk.
Wakati akinieleza hivyo simu yake ikaita, akapokea na kuanza kuzungumza na mtu aliyempigia ambapo nilimsikia akimwambia wapande ghorofa ya juu kabisa.
Hazikupita dakika tatu walifika vijana wawili, tuliposalimiana nao mmoja wao akasema;
“Bosi tumepata viwanja vitatu vizuri nadhani utavipenda kwani vipo sehemu nzuri.”
Baada ya yule Mwarabu kuambiwa hivyo, alifurahi sana na kuwaeleza kuwa waondoke waende wakavione ndipo walimalizia vinywaji na kuniambia niendelee kunywa chai, wakashuka chini.
Hata hivyo, dakika tano baadaye mmoja wa wale vijana alirudi na kuniambia kwamba bosi wao alisema haikuwa vizuri kuniacha peke yangu hivyo alinifuata.
Tulipofika chini tuliingia kwenye gari tukaondoka kuelekea sehemu iliyokuwa na viwanja hivyo, kwa kweli vilikuwa kwenye maeneo mazuri ya kujenga sheli.
Wale Waarabu walifurahi ndipo yule tajiri alisema turudi hotelini, tukaingia tena kwenye gari lake na kuanza safari.
Tulipofika tulikwenda kukaa sehemu tuliyokaa awali ndipo alifungua pochi yake akatoa kitita cha noti ambapo alihesababu shilingi laki mbili akanikabidhi.
Baada ya kunikabidhi aliniomba msamaha kwa usumbufu wote kisha akaniambia nirudi nyumbani nikaendelee na kazi zangu.
“Kijana utanisamehe kwa kukusumbua ila kwa kuwa kwako napajua nitakuja kukutembelea siku nyingine,” David anasema yule Mwarabu alimwambia.
Kwa kuwa biashara iliingia nuksi, niliwaaga nikateremka chini lakini nikajiwa na mawazo kwamba nisirudi nyumbani badala yake nitafute chumba cha kupanga kisha nitafute kibarua chochote.
Baada ya kufikiria hivyo nilikwenda mtaani ambako nilimuuliza kijana mmoja kama naweza kupata chumba cha kupanga akaniambia kuna mzee mmoja alikuwa na vyumba, akanipeleka.
Tulipofika tulimkuta mzee huyo aliyekuwa akiishi na familia yake na baada ya salamu yule kijana alimwambia shida yangu, akakubali kunipangisha chumba.
Kwa kuwa nilikuwa nina fedha siku hiyohiyo nilimlipa kodi ya miezi sita, nikanunua kitanda, godoro, blanketi, shuka moja, ndoo ya kuogea na ya kuwekea maji ya kunywa na vikombe viwili.
Siku iliyofuata ilipofika saa tatu asubuhi nilikwenda kwenye ile hoteli aliyonipeleka yule Mwarabu kwani niliamini nisingeweza kukosa kazi ya kufanya.
Nilipofika katika hoteli hiyo nilimfuata meneja na kumweleza shida yangu ambapo alinifahamisha kwamba hapakuwa na nafasi ya kazi.
Aliponipa jibu hilo nilifedheheka sana na kumsihi anipe kazi yoyote ningeifanya kwa bidii, meneja huyo alitulia kwa muda kisha aliniuliza kama naweza kufua nguo, nikamwambia naweza.
Baada ya kumpa jibu hilo aliniambia nitakuwa nasaidiana na kijana mmoja kufua mashuka, nilimshukuru sana kwa msaada wake.
Meneja huyo aliniambia kwa mwezi atakuwa ananilipa shilingi 65,000, kwa kuwa sikuwa na familia nikakubaliana naye.

Je, baada ya David kupata kazi katika hoteli ile kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, ushauri tuwasiliane kupitia namba hizo hapo juu.

No comments:

Post a Comment