Monday, March 25, 2013

Yanga: Tutawachezesha gwaride maafande Polisi Moro

Na Lucy Mgina
KLABU ya Yanga imesema itahakikisha inaendeleza wimbi la ushindi kwa kuifunga Polisi Morogoro Jumamosi ijayo.
Timu hizo zinatarajia kuvaana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro zikiwa na malengo tofauti. Yanga inataka ubingwa, wakati Polisi inapigania kutoshuka daraja.   
Yanga mpaka sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 48  huku Polisi ikiwa na pointi 17 katika nafasi ya tatu kutoka mkiani.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kikosi chao kimeimarika zaidi na kina ari ya ushindi katika mchezo huo ambao ni muhimu kwao kushinda ili watangaze ubingwa mapema.
Alisema mashabiki waendelee kuiunga mkono timu hiyo kwani siku hiyo lazima wawachape maafande hao na kuendeleza wimbi la ushindi.
“Kikosi kipo vizuri ila jana na leo (wikiendi) wachezaji wamepewa mapumziko na kesho (leo) wataanza mazoezi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama (Dar) kama kawaida.
“Ni lazima tuendeleze wimbi la ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa mapema zaidi, kwani msimu huu tumedhamiria kuhakikisha tunawapa raha zaidi mashabiki wetu,” alisema Kizuguto.

No comments:

Post a Comment