DKT. MVUNGI AFARIKI DUNIA AFRIKA YA KUSINI
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi, amefariki dunia jana
alasiri nchini Afrika Kusini, katika Hospitali ya Milpark, Johannesburg.
Dkt. Mvungi ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama
cha NCCR-Mageuzi na Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria Chuo Kikuu cha
Bagamoyo (UB), alipelekwa nchini humo baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa
usiku wa kuamkia Novemba 3 mwwaka huu akiwa nyumbani kwake, Kimbamba
Msakuzi.
Chama cha NCCR-Mageuzi, kimethibitisha juu ya kifo hicho na
kuongeza kuwa, taarifa kamili zitatolewa leo Makao Makuu ya chama
yaliyopo Ilala, kuanzia saa tatu asubuhi.
Mtoa habari hizo ndani ya
chama ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema marehemu
Dkt. Mvungi alikuwa kiongozi mkubwa ndani ya chama na ametumia fursa
hiyo kukifanya chama hicho kiwe na wanachama wengi.
Dkt. Mvungi
baada ya kujeruhiwa kwa mapanga, alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa
Tumbi, iliyopo Kibaha, mkoani Pwani na baadaye kuhamishiwa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi
Maalumu (ICU).
Kutokana na hali yake kutoimarika vizuri akiwa
hospitalini hapo, Novemba 7 mwaka huu, Dkt. Mvungi alisafirishwa kwa
ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink, kwenda Afrika Kusini
kwa matibabu zaidi hadi mauti yalipomkuta wakati madaktari wakiendelea
kuokoa maisha yake.
Msemaji wa Kitengo cha Taasisi ya Mifupa (MOI),
Bw. Jumaa Almas, alisema walilazimika kumsafirisha Dkt. Mvungi kutokana
na afya yake kutoimarika vizuri.
Dkt. Mvungi alipata majeraha
makubwa kichwani ambapio katika msafara wake, aliongozana na Daktari
Bingwa wa Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu Dkt. Clement Mugisha na
Muuguzi, Bi. Juliana Moshi.
Juzi Jeshi la Polisi nchini kupitia
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alisema watu
tisa ambao walihusika kumpiga, kumjeruhi na kuiba vitu mbalimbali vya
marehemu Dkt. Mvungi, tayari wamekamatwa.
Dkt. Nchimbi alisema watu
hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa nyakati
tofauti ambapo awali walikamatwa sita na juzi kufikia tisa.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, ambaye
alikuwepo katika mkutano huo, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Msigwa
Mpopela (30), Shabago Magozi na Hamadi Ally, jina maarufu 'Hatibu'.
Wengine
ni Zakaria Raphael (dereva wa bodaboda), Mmanda Saluwa, Juma Hamisi,
Longisho Semeriko (muuza ugolo), Paul Jeirosi na mwingine aliyemtaja kwa
jina moja la Kilimimazoka, ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam
"Watuhumiwa
hawa walikutwa na mapanga, kigoda ambavyo vimethibitika kuwa vilitumika
katika tukio hilo, pia walikutwa na simu ya mkononi mali ya Dkt.
Mvungi," alisema.
Kamishna Kova alisema, katika mahojiano ya awali
na watuhumiwa, walikiri kuhusika na tukio hilo na ushahidi umekamilika
kwa asilimia 80.
"Watuhumiwa wote wamekiri kosa hivyo tunakamilisha upelelezi ili wafikishwe mahakamani mara moja," alisema.
Marehemu Dkt. Mvungi, aliwahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi.
No comments:
Post a Comment