Saturday, February 28, 2015

ELEWA NI KWANINI WALIOFANIKIWA WANAENDEA KUFANIKIWA ZAIDI.


ELEWA NI KWANINI WALIOFANIKIWA WANAENDEA KUFANIKIWA ZAIDI.

Naomba kukiri kitu kwanza, wakati unaendelea kutafuta wazo la kibiashara, mbinu au maarifa ya kufanya jambo fulani la kuongeza kitu kwenye maisha yako, vipo vitu vichache sana ambavyo watu waliofanikiwa huwa wanavipa mkazo sana ili kuendelea kufanikiwa zaidi. Na vitu hivi vichache watu hawa huvipa uzito wa kipekee na kuvifanya kazi kwa umakini mkubwa, vitu hivi viko vitatu na leo tutaviangalia kwa undani kabisa.

Wana washauri wa maana; watu wote waliofanikiwa sana ukiangalia utagundua kuwa wamezungukwa  na washauri wa maana. Washauri hawa huwa walimu na viongozi wa watu hawa, watu hawa huwa na taarifa zote za msingi juu ya mambo anayofanya mtu huyu aliefanikiwa. Kama ni biashara basi watahakikisha wanakuwa na taarifa zote za washindani wake, taarifa hizi huwa ni muhimu kwasababu zinawasidia kujua washindani wao wanatumia mbinu na maarifa gani kwenye biashara zao, taarifa hizi wakizifanyia kazi huwa zinawaongezea mafanikio kwasababu watakuja sokoni na kitu ambacho ni cha tofauti na washindani wao.Washauri na wataalamu hawa huwa wanatumika kwenye kila sekta, ukiangalia wanamichezo, wanamuziki, viongozi wa makampuni na hata wajasiriamali waliofanikiwa sana utaona wamewaajiri wataalamu hawa na wanawalipa fedha nyingi sana ili tu waweze kuwapatia taarifa na ushauri utakao waongezea mafanikio. Unahitaji kuyafahamu na kuyaelewa haya wakati unatafuta mafanikio yako binafsi na hata yale ya kibiashara, lakini pia ni hekima kubwa kuelewa ni kiasi gani utaathirika endapo utakosa washauri wazuri wa kukusaidia. Muda mwingine huwa tunafanya jambo vibaya au chini ya kiwango bila kuelewa, kwahiyo unahitaji mtu mwingine wa pembani akueleze na kukuonyesha ni wapi unakosea na nini ufanye ili mambo yabadilike kwenda muelekeo sahihi. Hivyo ni muhimu sana kuzungukwa na watu waliokuzidi mbinu, maarifa na zaidi sana uzoefu ili wawe msaada pale ambapo unakosea na kuhitaji msaada, na watu hawa ni kuwaheshimu na kuwajali sana kwani ukiwapoteza inakuwa ni hasara kubwa sana kwako. Kama unataka kubadilisha maisha yako hakikisha unatafuta washauri na wataalamu wazuri wa kukusaidia na kukuongoza kuyafikia malengo yako.

Wana mtandao wa watu wa maana; licha ya kuwa na washauri wazuri lakini pia watu hawa huwa na mtandao mpana wa watu wa maana, watu wa maana ni wale ambao mnawaza na kuwa na malengo sawa, watu hawa huwa ni muhimu kwa sababu mara nyingi wanaelewa nini cha kufanya na kwa wakati muafaka. Sisi kama binadamu ni asili yetu kufanya mambo kwa kiwango na uwezo wa watu waliotuzunguka, mtaalamu mmoja alisema, ukitembea na mtu mwenye mwendo mkubwa kuliko wa kwako itakubidi wewe uongeze mwendo wako ili muwe sawa, kwa mara ya kwanza itakufanya ujisikie tofauti au hata vibaya lakini baada ya muda utaizoea ile hali na hatimaye kuwa nae sawa. Vivyohivyo ukitembea na mwenye mwendo mdogo utajikuta na wewe unapunguza mwendo wako unapungua ili uendane na wa kwake, ukweli ni kuwa watu waliokuzunguka wanatosha kabisa kukufanya ufanikiwe au usifanikiwe, hebu angalia umezungukwa na watu wa aina gani. Wataalamu wengi sana wameandika na kufanya tafiti mbalimbali juu ya jambo hili na wote wamefikia kwenye hitimisho moja, wanasema watu wengi wanaoyatafuta mafanikio wemeshindwa kuyafikia malengo yao kwa sababu hawajazungukwa na watu wenye malengo kama yao au wenye malengo makubwa zaidi yao. Usishangae kuona waliofanikiwa sana kuwa na marafiki wachache lakini wa maana, usishangae ni kwanini huwa wanaunda chama au asasi ambayo huwa wanakutana kwa ajili ya kubadilishana mawazo, usishangae ni kwanini wanakuwa kwenye bodi za makampuni makubwa, ukweli ni kwamba wanafanya hivi ili waweze kukutana na watu wenye mitizamo na mawazo kama ya kwao. Kama unataka kubadilisha maisha yako hakikisha unakuzungukwa na watu wenye malengo, mitazamo na mawazo kama ya kwako.

Wana mipango na mikakati; watu waliofanikiwa sana wana mipango, mikakati na mifumo ambayo inawawezesha kufanya mambo kwa kiwango kikubwa kuliko watu wa kawaida na wale wa chini kabisa. Watu wengi huwa wanajaribu tu na kufanya mambo bila kujiandaa, wanakosa mipango na mikakati madhubuti yenye uhakika wa kuleta matokeo mazuri na makubwa. Mtaalamu mmoja anasema, “Ukiweza kufanikisha jambo moja, unaweza pia kufanikisha mambo mengine mengi kwa kufuata mipango na mikakati ileile”.  Ukitaka kubadilisha maisha yako utahitaji kuzielewa taratibu, uwe na mikakati madhubuti pamoja na mfumo unaoeleweka.

Ili uwe na uwanja wa mafanikio sawa na matajiri na wengine waliofanikiwa sana kwenye mambo yao, ni muhimu sana kuvielewa na kuvifanyia kazi hivyo vitu vitatu hapo juu. Kumbuka pia watu wenye vitu na maisha ambayo wewe huna wanaelewa na kufanya mambo ambayo wewe huyajui na kuyafanya, ukitaka kufanikiwa angalia waliofanikiwa wanafanya nini na wewe ufanye, hakuna siri kwenye mafanikio zaidi ya kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa.

No comments:

Post a Comment