Thursday, March 19, 2015

Mengi yafichuka ajali ya gari Mafinga.

*zaidi ya moja, basi lile lile dereva yule yule.
*Sifa ya dereva wa mabasi eti ni mwendo kasi.
AJALI iliyotokea eneo la Changarawe, Mafinga Jumatano iliyopita, bado ndiyo habari yenye kuendelea kujadiliwa kila kona ya Mkoa wa Mbeya.
Ni ajali iliyoua watu 50, leo hii ni vilio kila kona ya Jiji la Mbeya. Ni wazi itaendelea kubaki katika kumbukumbu za wakazi wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe kwa miaka mingi ijayo.
Watu wengi waliofariki katika ajali hiyo ni wakazi wa Jiji la Mbeya, lakini wenye kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya yenyewe.
Siku za Ijumaa, Jumamosi na hadi Jumapili zilikuwa na pilikapilika za kusafirisha miili ya marehemu na mazishi, kutoka Mafinga hadi Mbeya na baadaye kwenye maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo kwa ajili ya mazishi.
Nini hasa sababu ya ajali?
Ni swali lenye kuumiza vichwa vya wakazi wa Jiji la Mbeya na ndilo lililotawala mazungumzo ya wakazi wa jiji hilo, tangu kutokea kwa ajali hiyo.
Mengi yamezungumzwa kuhusiana na ajali hiyo, wapo wenye kuamini kuwa imesababishwa na ushirikina, wakiamini kuwa ni ajali iliyohusishwa na utoaji kafara. Hawa yawezekana ni kutokana na kutoamini kwamba yawezekana kutokea kwa ajali kama ile, yenye kuteketeza watu wengi kwa wakati mmoja kutokea.
Lakini zipo sababu za kisayansi zenye kutumika kuielezea ajali ile, zikiwemo mwendo kasi, ubovu wa barabara na uzembe. Hata hivyo, sababu kuu iliyozungumzwa zaidi ni ubovu wa barabara, kwamba ajali ilisababishwa na dereva wa lori alipolazimika kulikwepa shimo kwenye eneo hilo la barabara.
Miongoni mwa wenye kusimamia sababu ya ubovu wa barabara ni pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa, Ramadhan Mungi, ambaye alinukuliwa akisema: “Hapa tusitafute mchawi, katika hii ajali chanzo kikubwa ni ubovu wa barabara, hivyo ni jukumu la mamlaka husika kurekebisha.”
Pamoja na kukubaliana na sababu hiyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya ajali za barabarani, wakiwemo abiria, madereva na askari wa usalama barabarani, wanaelekeza lawama zote kwa madereva wote wawili, basi la abiria na lori.
Wachambuzi hao wanaamini kwamba, iwapo madereva wote wawili wangekuwa makini na kazi yao, ile ajali isingetokea, kwamba walikuwa na nafasi kubwa ya kuiepuka.
“Kilichotokea, madereva wote wawili walipigiana hesabu, waliachia, magari yalikuwa katika mwendo wa kasi, kila mmoja akiamini atamuwahi mwenzake,” anasema dereva mmoja wa magari makubwa ya mizigo.
Kwa mujibu wa madereva wa magari makubwa, waliozungumza na Raia Mwema, ni kawaida ya madereva, hasa wale wenye magari yaliyochoka, “kuchochea” mwendo kwenye mteremko ili iwe rahisi kupandisha mlima ulio mbele yake.
Mazingira ya eneo lilipotokea ajali, ni kwamba wote wawili, lori na basi walikuwa kwenye mteremko huku wakikabiliwa na mwinuko mbele yao.
Hoja nyingine inayotumika na wachambuzi hao ni kwamba hilo eneo lipo siku zote na magari yanapita saa zote na kwamba hata kabla ya ajali hiyo, yamepita mabasi mengi tu ya abiria na magari ya mizigo na wameweza kupishana vizuri tu, sababu ya kutosababisha ajali ikiwa ni umakini wa madereva.
“Shimo ni kisingizio, kama ni hivyo basi zingetokea ajali hata kwa waliotangulia, hazikutokea kwa sababu madereva walikuwa makini, walizingatia sheria zinazowaongoza barabarani,” anasema mfanyabiashara mmoja wa magari makubwa aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwakapijila.

Wachambuzi hao wanabainisha kuwa endapo uchunguzi utafanyika ipasavyo, udhaifu utabainika kwenye lori la mizigo lililosababisha ajali ile, kwamba hatua ya dereva wake kuongeza mwendo akiwa kwenye mteremko ili apande kwa urahisi mwinuko aliokuwa akiukabili mbele yake ni ushahidi kwamba gari halikuwa na nguvu, hivyo halikuwa katika hali nzuri.
Pia inabainishwa kuwa hatua ya dereva wa basi kuchochea mwendo wakati analiona lori linakuja kwa kasi, inajenga shaka katika uwezo wa dereva yule kwenye uendeshaji, hakupaswa kupiga hesabu za kuwahi, alikuwa na nafasi ya kuepusha ajali iwapo angetumia busara.
Katika mijadala hiyo, inaibuka hoja nyingine kumhusu dereva wa basi, ikielezwa kuwa takribani siku 10 kabla ya ajali hiyo ya Mafinga, alisababisha ajali nyingine katika eneo la Mafiat, jijini Mbeya akiendesha basi lile lile.
Dereva yule yule, basi lile lile, ajali zaidi ya moja ndani ya muda
mfupi, ni wazi kwamba kuna udhaifu mahali, kuanzia kwa mmiliki wa basi lenyewe hadi wasimamizi wa sheria.
Sifa kuu ya dereva yule ni kwenda mwendo wa kasi, ni wazi mmiliki alilifahamu hilo na ndio maana alimpenda sana, hata pale aliposababisha ajali aliendelea kumwamini.
Imani ya mmiliki kwa dereva yule inadaiwa kwamba haitokani na elimu pamoja na uzoefu, bali ni kuwahi kufika, akiyapita mabasi yaliyomtangulia kuondoka kituoni.

Dereva asiye na shinikizo la kuwahi kufika kuliko wenzake wote, afikapo eneo “korofi” kama la pale Changarawe hupunguza mwendo na huanzia mbali kupunguza, wala kutoingia kwenye mashindano na wenzake, wenyewe huita ligi.
Yapo mabasi, abiria wanaelezwa kabisa, mathalani kampuni ya Ndenjela, safari za Mbeya na Dar es Salaam, sio chini ya saa 12. Msingi wa mmliki huyo kuweka msimamo wake huo kwa mabasi yake ni kwamba, pamoja na umbali, magari ya mizigo ni mengi sana katika barabara kuu hiyo ya Dar es Salaam - Mbeya.
Mkoa wa Mbeya ni lango la kuelekea nchi zilizoko Kusini na Kusini Magharibi mwa Afrika, ikiwa na mipaka miwili, Kasumulu wilayani Kyela na Tunduma wilayani Momba, huku shehena kubwa ya mizigo kwenda nchi hiyo ikisafirishwa kwa njia ya barabara.
Hatua za kuepusha ajali kubwa
Pamoja na ubovu wa kipande cha barabara hiyo, kutoka Mafinga mkoani Iringa hadi Tunduma mkoani Mbeya, lipo tatizo jingine la ufinyu wa barabara barabara hiyo. Inahitaji utulivu na umakini sana katika kupishana kwenye barabara hiyo, kuyumba kwa gari moja lazima kutasababisha ajali.
Hata hivyo, upanuzi na ujenzi mpya wa barabara hiyo hautasaidia iwapo utoaji leseni hautadhibitiwa, kwamba mbeba mizigo kwenye basi (utingo), anajifunza kuendesha basi kwa huruma ya dereva wa basi, kisha anakabidhiwa basi la abiria 65, sio utaratibu mzuri.
Ukaguzi wa muda unaotumika uimarishwe, haingii akilini basi lililoachwa kituoni kwa nusu saa liwe la kwanza kufika, kwani mzingira ya barabara hiyo hayaruhusu mwendo wa kasi.
Wapo wadau wenye kuamini kuwa adhabu zinazotolewa kwa kampuni za mabasi yenye kusababisha ajali hazina maumivu. Wanapendekeza kutumika zaidi adhabu ya kunyang’anywa leseni kwa kampuni yenye kubainika kukiuka sheria, hususani zihusuzo uimara wa basi na ajira ya madereva.
Wakati umefika kwa serikali kusikia kilio cha muda mrefu cha wananchi kuhusu matumizi ya Reli ya TAZARA kusafirisha mizigo badala ya barabara.
Wananchi mkoani Mbeya wanamini kuwa Reli ya TAZARA haina tatizo la miundombinu, tatizo lake kuu ni utawala, hivyo ukiboresha utawala na uendeshji wa Mamlaka hiyo , itaweza beba asilimia kubwa ya mzigo hivyo kuondoa msongamano barabarani pamoja na kuokoa barabara.
Ni jambo lenye kushangaza kuona mitambo, mataruma na mizigo mingine mizito ikisafirishwa kwa njia ya barabara. Hatua iliyofikia barabara hiyo inatisha, na wala uhitaji kwenda mbali kujionea huo ubovu, kipande kinachokatisha kwenye jiji la Mbeya pekee kinathibitisha jinsi barabara hiyo ilivyoharibika.
Wananchi wamejenga imani kwamba viongozi wanahujumu reli ili waendelee na biashara yao ya magari makubwa ya mizigo. Ili kujinasua na tope hilo, ni wakati sasa wa uongozi wa nchi kufufua usafiri wa reli.
Chanzo,Raia Mwema.

No comments:

Post a Comment