Siku aliyonipa ofa ya pombe ndiyo ukawa mwanzo wa kunisumbua kimapenzi, kwa kweli nilijitahidi sana lakini nilijikuta nimemkubalia bila kujua. Naomba mume wangu usiniache, mama alishaniambia siku nikifanya ujinga kwako na wewe kunifukuza, basi nitafute pa kwenda nisirudi kwake.
SASA ENDELEA...
“Nakuahidi mume wangu sitafanya ujinga tena na pombe leo ndiyo mwanzo na mwisho.”
Japo kauli ya mke wangu haikuwa na nguvu ya kunishawishi kumsamehe hasa baada kujua kuwa ametoka kwa mwanaume baada ya kunikimbia kitandani na kwenda kufanya uchafu wake. Kikubwa kilichoniuma ni dharau zilizokuwa zikioneshwa na jirani yangu kwa kutembea na mke wangu akijua ni mke wa mtu.
Kilichoniuma zaidi kilikuwa kumshawishi kunitoroka kitandani na kuniacha peke yangu.
Roho iliniuma kufanywa bwege kiasi kikubwa, kwangu ilikuwa dharau kubwa sana ambayo iliuumiza moyo wangu kwa jinsi nilivyodhallishwa kiasi cha kutaka kulipa kisasi cha historia.
Niliamini kuwa mke wangu hakuwa na kosa ila kuna watu walitaka kuniona mimi ni nani. Nilipanga mwisho wa wiki niende tena kwa babu kumtia adabu.
Tena mtu huyu sikuwa na huruma naye hata kidogo niliapa kumbakisha jina tu.
Nilimsamehe mke wangu na kumuomba abadilike la sivyo sitamuuliza kitu chochote tena na wala sitamfukuza.
Mke wangu alinihakikishia kutulia kwa kusema kuwa hatarudia tena kosa kama lile, siku ile niliiacha ipite lakini moyoni nilikuwa na maumivu na hasira kama nyoka aliyekanyagwa mkiani.
Nilijitahidi kuficha kilichonikuta kwa watu wote huku nikiomba mwisho wa wiki ufike upesi.
Siku zote mke wangu hakuacha kuniomba msamaha, nilimwa,bia kuwa nimemsamehe toka moyoni na si mdomoni.
Jirani yangu baada ya kugundua nimegundua hila zake ya kumchukua mke wangu, akawa anatoka alfajiri na kurudi usiku wakati siye tukiwa tumelala. Moyoni nilijisemea kuwa arukeruke lakini siku zake za kuishi duniani zilikuwa zinahesabika, nikifika kwa mzee Kidereko lazima alambe udongo.
Niliapa kuwa siri ile hataijua mtu yeyote, baada ya kumsamehe mke wangu nilijilazimisha kuishi maisha ya kulazimisha furaha huku moyoni nikiwa na maumivu makali kutokana na tabia za watu kumgeuza mke wangu jamvi la wageni.
Kwa vile dawa yao niliijua sikutaka kubishana na mtu zaidi ya kupanga safari ya kwenda kwa Mzee Kidereko kule Tewe.
Hakuna aliyegundua mabadiliko yangu kazini na nyumbani, wengi walijua uhusiano wetu ulikuwa ni mzuri, pia kitabia mke wangu alikuwa amejirekebisha.
Hata safari yangu ya kwenda Tewe niliifanya kuwa ni siri yangu, sikutaka kumwambia hata Shedu aliyenipeleka kwa mzee Kidereko kwa mara ya kwanza.
Moyo wangu ulikuwa umeingia woga kuiogopa aibu ya kuonekana bwege kama watu wangejua kuwa mke wangu karudia makosa yaleyale.
Ijumaa baada ya kazi nilianza safari yangu huku nikimuaga mke wangu kuwa nakwenda nyumbani kwa wazazi nimeitwa mara moja. Mke wangu alinitakia safari njema huku akinihakikishia kwa maneno mazito kuwa nimuamini.
“Mume wangu najua huniamini tena moyoni mwako, lakini nakuahidi mbele ya muumba ambaye hakosekani kila sehemu, yeye ndiye shahidi yangu kwa haya ninayoyasema mbele yako muda mfupi kabla hujaenda kuwaona wazazi wako.
“Ni kwamba nimekuwa kama kaniki isiyobadilika rangi hata ukifuliwa na kusuguliwa vipi.
“Lakini hili ninalolisema mbele yako kama nitarudia tena kosa basi Mungu anigeuze kiumbe chochote cha ajabu au kuyachukua maisha yangu,” mke wangu alisema kwa sauti iliyotia uchungu.
Alizungumza maneno mazito ambayo yalinitoa machozi na kunifanya niamini kuwa kiapo chake kile kilitoka moyoni mwake na kujutia alichokifanya.
Pamoja na kutaka kumuamini bado nilimuona kama mjusi asiyeweza kugeuka kuwa nyoka hata ukimpaka unga.
Nilijua kile kilikuwa ni kilio cha majuto lakini mke wangu alikuwa na akili za mbuzi, hakawii kujisahau na baada ya tukio hutulia na kujutia.
Kwa upande mwingine kiapo cha mke wangu nilikiona kizito sana kwa kuwa alijichagulia adhabu na kama atarudia utakuwa ni upumbavu wake.
Wazo la kusitisha safari yangu lilikuja na kuona hakuna haja ya kwenda kwa mzee Kidereko, niliona ni heri nitulie tu na kufanya mambo mengine.
Nini kiliendelea? Usikose Jumatano kusoma kwenye Risasi Mchanganyiko.
No comments:
Post a Comment