Sunday, April 14, 2013

WAMELEA WENYEWE... SASA NAO MASTAA


Na Gladness Mallya
ULIMWENGUNI kuna mambo mengi ya kuhuzunisha na kufurahisha hasa ukipata kusimuliwa maisha ya mtu mmoja baada ya mwingine. Bongo kuna akina mama watatu ambao ningependa kuwazungumza katika makala haya. Kwa vyovyote ukimaliza kusoma ukurasa huu utakuwa na jambo la kujifunza, uchukue hatua.
Mama mzazi wa Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim ‘Sandra’.
Akina mama hawa, waliwalea watoto wao wenyewe kwa kipindi kirefu cha maisha yao bila baba zao lakini sasa wanafurahia matunda mazuri kutoka kwao. Nao wamekuwa mastaa. Shukrani kwa kazi za sanaa za watoto wao.
Nawazungumzia mama wa mwanamuziki anayeuza zaidi wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aitwaye Sanura Kassim ‘Sandra’, mama wa mwigizaji sistaduu, Wema Isaac Sepetu ‘Beautful Onyinye’, Miriam Sepetu na mama wa aliyekuwa mwigizaji mkubwa Bongo, marehemu Steven Kanumba ‘The Great’, Flora Mtegoa.
MAMA DIAMOND
Baada ya mwanaye Diamond kutusua kupitia Bongo Fleva naye alipata umaarufu kutokana na kuonekana mara kwa mara akifuatana naye katika shoo zake na kwenye kumbi mbalimbali za starehe. Mama Diamond anazijua kamera za waandishi. Anajua kukatiza kwenye zulia jekundu akiwa na mwanaye hivyo wakati wa matumizi ya picha hizo katika vyombo vya habari, kumkwepa huwa vigumu.
HISTORIA
Mama Diamond alikuwa akiishi na baba Diamond, Abdul Jumaa, alipata ujauzito na kufanikiwa kujifungua salama. Baada ya mtoto Diamond kuzaliwa, visa vya hapa na pale vilianza kwani wakwe zake ‘yaani upande wa bibi yake Diamond, mzaa baba’ walikuja juu na kumtaka mtoto wao aachane na mama Diamond ambapo walimtafutia mwanamke mwingine na kumuoa.
Baada ya baba Diamond kuoa, mama Diamond na mwanaye walirudi nyumbani kwa wazazi wake, Tandale, Dar. Huko mama Diamond alimlea mwanaye kwa shida. Mara kadhaa Diamond amekuwa akilia anapokumbuka alikotoka kimaisha na mama yake bila msaada wa baba hadi alipokuwa mkubwa.
Tangu akiwa mdogo alianza kurap huku mama yake akimpeleka katika matamasha mbalimbali ya muziki akimuombea kwa wadau apate nafasi ya kuonesha kipaji chake.
Kurap ikashindikana. Diamond akaanza kuimba, akachomoka kimuziki, akatwaa tuzo akawa anapata mashavu ya shoo ndani na nje ya nchi. Hapo ndipo mama Diamond alipopata ustaa na sasa anafurahia matunda ya mwanaye. Tayari anajua kucheza na kamera, anaweza kutatua tatizo la kukosekana kwa akina mama katika tasnia ya filamu. Ni kiasi cha kuamua tu!
Mama mzazi wa Wema Isaac Sepetu ‘Beautful Onyinye’, Miriam Sepetu.
MAMA WEMA
Mama Wema alipata umaarufu mkubwa kutokana na vimbwanga vya mwanaye mara tu baada ya kutwaa taji la Miss Tanzania 2006/07. Mara kadhaa alionekana runingani na inaaminika kuwa ustaa alionao unatosha kumpa ulaji katika tasnia ya filamu za nyumbani endapo tu ataamua.
HISTORIA
Uchunguzi unaonesha kuwa katika kipindi chote cha umaarufu wa Wema, mama yake ndiye aliyekuwa na jukumu la kumlea staa huyo wa filamu za nyumbani. Habari za uhakika ni kwamba mama Wema anaishi bila baba Wema kwa kipindi kirefu. Baba Wema yupo Zanzibar. Hata hivyo, chanzo cha kila mmoja kuishi kivyake hakijafahamika. Mara ya mwisho baba Wema alionekana na familia yake Tanzania Bara mwaka 2006 wakati mwanaye huyo alipotwaa taji la Miss Tanzania. Uchunguzi unaonesha kuwa alikuja baada ya kuombwa na Mratibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga aliyemtumia tiketi ya ndege.

No comments:

Post a Comment