Sunday, August 5, 2012

HATARI! Nguvu zaidi zinahitajika kupambama na ebola


Kuingia kwa ugonjwa wa ebola hapa nchini katika Mkoa wa Kagera ambapo mtoto mmoja wa miaka sita anadaiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Ugonjwa huo unaripotiwa kutokea nchini Uganda ambako mpaka sasa umeua watu 14 na sita wanaendelea na matibabu huku wataalamu wakihangaika kuzuia maambukizi yake.
Taarifa hizi zinakuja siku chache baada ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutoa tahadhari juu ya ugonjwa huo hasa kwa wakazi wa mikoa iliyo jirani na Uganda ambayo ni Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma na Rukwa.
Kwa mujibu wa taarifa za wizara, chanzo chake ni virusi vya ebola na dalili zake ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa, na vidonda kooni.
Wataalamu wa afya wanabainisha kuwa dalili hizo mara nyingi hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa damu ndani na nje mwilini.
Wataalamu hao pia wanasema ugonjwa huo huenea kwa maambukizi ya kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa njia za kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huona kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huu.
Ebola pia humpata mtu aliyegusa wanyama walioambukizwa (mizoga na wanyama hai) kama sokwe na swala wa msituni.
Wizara ya Afya imedokeza kuwa ugonjwa huo mpaka sasa hauna tiba wala chanjo, hivyo ni vema wananchi wakawa makini na ugonjwa huo hasa wanapomuona mtu mwenye dalili hizo.
Taarifa za ugonjwa huu zimetushtua sana kwakuwa wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya masuala ya afya na maeneo mengi yapo mbali na vituo vya afya.
Tungependa serikali iweke nguvu nyingi na ikiwezekana ipeleke wataalamu zaidi wa afya kwenye maeneo yaliyo na hatari ya kuupata ugonjwa huu.
Tumezoea kuiona serikali ikifanya kazi kwa utaratibu wa zima moto, ambapo hungoja mpaka jambo litokee ndipo hutuma wataalamu wake kwenye maeneo husika.
Tunaamini kuwa huu si wakati wa kufanya kazi kwa mazoea, ugonjwa wa ebola ni hatari hivyo hata mapambano yake yanahitajika yawe makubwa zaidi.
Serikali isipofanya jitihada kubwa katika kupambana na ugonjwa huo watu wengi watapukutika, wananchi wanaitegemea zaidi serikali iwanusuru katika janga hili.
Tunawaomba wananchi watoe taarifa kwa waganga wakuu wote wa mikoa na wilaya walio karibu nao mara wanapoona kuna mtu ana dalili hizo kama ilivyofanyika huko Kyerwa.

No comments:

Post a Comment