Friday, August 24, 2012

SIMBA SC YAWAWEKEA PINGAMIZI TWITE, YONDANI


Na Wilbert Molandi

UONGOZI wa Simba, juzi ulipeleka pingamizi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusu kunyimwa uhalali wa usajili wa mabeki Kelvin Yondani na Mbuyu Twite.
Wachezaji hao bado wanaumiza vichwa vya Simba. Inaelezwa kuwa Yondani amesajiliwa na Yanga akiwa ndani ya mkataba wa Simba, wakati Twite alirudisha fedha za usajili za Wekundu hao akiwa amesaini mkataba na kutimkia Yanga.
Kamati ya Katiba, Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF inayoongozwa na Alex Mgongolwa, hivi karibuni iliidhinisha uhalali wa wachezaji hao kuichezea Yanga, ikisema Simba haikufuata taratibu za usajili.
Simba wamepinga hilo na juzi walipeleka rasmi pingamizi katika ofisi za TFF, wakidai wana uhalali wa kuwatumia wachezaji hao, huku wakisisitiza hawana imani na baadhi ya wajumbe wa kamati ya Mgongolwa.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema: “Simba imewasilisha rasmi barua ya pingamizi, hatuna imani na baadhi ya wajumbe wa kamati ya sheria ambao ni Iman Madega, Lloyd Nchunga  na Mgongolwa.
“Tunataka wajumbe hao waondolewe na watafutwe wanasheria wengine wasiokuwa na mapenzi na Yanga wala Simba ili haki itendeke, kwa sababu kama Twite alichukua fedha na kusaini timu mbili ni lazima achukuliwe adhabu kwa mujibu wa sheria.
“Suala la Yondani ilikosewa tarehe tu, wakati Yanga wanamsajili alikuwa mali ya Simba, hata aliposajiliwa alikuwa amevaa jezi ya (Taifa) Stars, baada ya kumtorosha kambini. Tunaamini haki itatendeka kama sheria itafanya kazi yake,” alisema Kamwaga. 

No comments:

Post a Comment