KAMPALA ni mji mkuu wa Uganda, nchi jirani ya Tanzania upande wa kaskazini-magharibi. Je, unajua mji huo wenye watu wapatao 1,800,000 ulipataje jina lake?
Kabla ya mji huo kuanzishwa na Waingereza, eneo lake lenye milima na ardhi chepe, yaani yenye maji, lilikuwa ni makazi ya wanyama aina ya paa au swalapala ambao kwa Kiingereza huitwa ‘impala’.
Waingereza walipofika hapo wakapaita “The Hill of the Impala” yaani “Mlima wa Swalapala”.
Hivyo, Baganda (watu wa kabilala Kiganda) wakawa wanapaita “Akasozi k’empala” maneno yanayomaanisha pia kuwa “Mlima wa Swalapala”.
Kwa matamshi ya neno kwa neno maneno hayo yalibidi yatamkwe kama “Akasozi ka Impala”, lakini kwa matamshi ya jumla hutamkwa: “Akasozi k’empala”.
Kama kawaida – kwa makusudi au kwa bahati mbaya – neno “Akasozi” likaachwa na badala yake likabaki neno “K’empala” ambalo nalo baadaye matamshi ya watu mbalimbali yakalibadili neno hilo na kuwa “Kampala”.
Hivyo ndivyo jina Kampala -- mji wa Meya Erias Lukwago – lilivyopatikana!
Bila shaka watu wa Uganda wanakubaliana nalo, la sivyo wangetaka jina kamili la “Akasozi k’empala” lirudishwe.
No comments:
Post a Comment