Monday, November 19, 2012

UNAPOPEWA, JIULIZE UNATOA NINI? USIENDEKEZE MAPENZI YA KIZAMANI -5


LEO naendelea na ‘topiki’ hii niliyoianza wiki iliyopita inayohusiana na wapenzi kusaidiana na kuacha mapenzi ya kizamani ya kumtegemea mtu mmoja. Endelea...
Labda nisisitizie kitu, sina maana kwamba kama wewe unatoa fedha ni sharti naye awe anakupa, la hasha! Uhusiano bora wa mapenzi huboreshwa na namna ambavyo wahusika wanavyohudumiana. Kila mmoja kuhakikisha anakuwa jirani na mwenzake wakati wote.

Mmoja anaweza kuwa na matatizo ya kipato, ni vizuri sasa mwenzake kuwa naye karibu kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha. Ni ajabu pale mtu anapokabiliana na hali ngumu ya muda mfupi na anahitaji tu faraja kutoka kwa mwenzi wake lakini akawa hapati.
Hizo ndiyo dalili za unyonyaji. Kama wewe matatizo yako ya kifedha unayaweka mstari wa mbele na unatatuliwa, iweje mwenzako umeshindwa kumfariji wakati wa shida zake? Hiki ni kipengele kibaya ambacho kimewafelisha wengi. Baadhi wamepoteza wapenzi bora kwenye maisha yao.
KUNA MFANO KHALID NA GIFT
Khalid akiwa na upendo wa dhati kwa Gift, alimtabiria mema na kumtegemea kwamba ndiye atakuwa mke wake wa ndoa. Walipokuwa wanaanza uhusiano, Gift alikuwa amemaliza kidato cha sita Shule ya Sekondari Mwanza, wakati huo, Khalid alikuwa ni mfanyabiashara wa mitumba, Soka la Mlango Mmoja (Langolango), Mwanza.
Walifahamiana kwenye daladala, siku ambayo Khalid alimkuta Gift akiwa kwenye muonekano wa kukata tamaa ya maisha. Alikuwa amepata alama ambazo asingeweza kuendelea na chuo kwa udhamini wa serikali. Hilo lilimkatisha tamaa, ndoto zake za kuwa daktari bingwa wa kike aliona zimefika ukingoni.
Hata mwanzoni Khalid alipojitahidi kuzungumza na Gift amueleze tatizo lake, alimdharau. Alimuona wa kawaida, asingeweza kumpa msaada wowote. Kwa maana hiyo alimdharau lakini Khalid aliongeza juhudi kujua kilichopo ndani ya mrembo huyo.
Baada ya mzunguko wa muda mrefu, ikabidi Khalid aombe japo mawasiliano. Wakabadilishana namba za simu. Tangu siku hiyo, Khalid aliendelea kumfikiria sana Gift, aliwaza vitu vingi. Kubwa zaidi alihisi kuna  kitu kikubwa kipo ndani yake, alijihisi kumpenda mrembo huyo.
Kingine kilichomsumbua Khalid ni hali ya Gift, alihisi kuna tatizo kubwa ndani yake. Siku moja akamtafuta kwenye simu, alipompata alimuomba wakutane, akamkatalia. Akaendelea kumjaribu mara kwa mara, akawa anagonga ukuta lakini baada ya wiki mbili, Gift alikubali kukutana na Khalid.
Walikutana kwa mara ya kwanza Ilemela, Tunza Beach, wakazungumza mengi, wakaweza kufahamiana. Gift akatambua kwamba Khalid ni mfanyabiashara wa mitumba, vilevile Khalid akaelewa nini hasa kinachomtesa Gift. Khalid akaamua kulibeba tatizo la Gift kama lake.
Maisha yakaendelea, Khalid hakuwa mtu mwenye pesa nyingi lakini aliamua kutumia akiba yake kuhakikisha Gift anakuwa na furaha, anatimiza pia ndoto zake. Khalid alieleza ombi lake la kumtaka wawe na uhusiano wa kimapenzi na panapo majaliwa, waweze kufunga ndoa.
Gift ombi hilo alilikubali. Wiki moja baadaye, Khalid alimsafirisha Gift kwa ndege kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia nafasi za kujiunga na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Gift kusafiri kwa ndege, aliona ndoto, akamshukuru sana Khalid.
Alipata chuo, Khalid akamlipia ada, bweni na matumizi mengine. Kwa kifupi Khalid aligeuka baba kwa Gift, alimhudumia kila kitu. Gift alipopatwa na tatizo lolote, mtu wa kwanza kumpigia alikuwa ni Khalid ambaye alitatua bila kusita, akijua anajenga maisha ya mkewe mtarajiwa.
Kuna wakati ubinadamu ulimuingia Khalid, akawa anaomba kufanya mapenzi na Gift lakini hakufanikiwa. Siku zote Gift alimwambia asubiri mpaka watakapofunga ndoa. Japo Khalid ilimuuma lakini upande mwingine aliona msimamo wa Gift ni mzuri na alilegea kila alipokumbuka kauli tamu ya Gift: “Usijali mpenzi wangu, mimi ni wako, tutafanya mpaka utachoka.”
Siku, wiki, miezi, ikawa mwaka, miaka ikapita, Gift akamaliza chuo. Hakutaka hata kurudi Mwanza. Alichokikataa ni kuonana na Khalid. Alimuona mwanaume asiye na elimu, kwa hiyo kuwa na mume aina yake aliona kama ni kupoteza dira ya maisha. Wanaume wasomi ni wengi.
Khalid alijitahidi kufika Dar es Salaam, akaa mwezi mzima bila kuonana na Gift ambaye kwa kuona kero, akaamua kubadili na namba ya simu. Kutokana na uhusiano wao kutambuliwa mpaka na wazazi pamoja na ndugu wengine, aliwashirikisha lakini hakuna alichoambulia.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment