Thursday, December 6, 2012

UBONGO WA JAMBAZI ALIYEUAWA KWA RISASI WAGOMBEWA


Na Mashaka Baltazar, Mwanza
UBONGO wa mmoja wa majambazi waliouawa na polisi kwa kupigwa risasi eneo la darajani lililopo jirani na nyumba ya kulala wageni ya Mayolwa, Kilimahewa wilayani Ilemela, jijini Mwanza unadaiwa kuwa ni dili baada ya watu kuugombania.


Wiki mbili zilizopita jeshi la polisi jijini hapa, liliwaua watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na bunduki ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) ikiwa na risasi 43 na magazine mbili. 
Katika majibizano hayo, polisi waliwaua wawili kati ya majambazi watano ambapo mmoja alifumuliwa kichwa  kwa risasi na ubongo kumwagikia ndani ya mto.
Kufuatia tukio hilo, watu wasiojulikana waliingia mtoni na kuchota ubongo huo kisha kwenda kuuuza.
Ubongo huo uliodaiwa kuwa ni ‘dili’, ulinunuliwa kati ya shilingi 15,000 hadi 20,000 jambo lililowashangaza watu wengi jijini hapa.
Watu waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema hayo yote husababishwa na imani potofu za kishirikina.
Mmoja wa watu hao, alisema katika hali ya kawaida na kwa mtu anayemcha Mungu hawezi kununua ubongo wa binadamu kwa madai kwamba ni dawa ya kupata mali au kuutumia kufanyia mazindiko.
“Ni ujinga na upuuzi wa hali ya juu kuamini kupata utajiri kwa kutumia ubongo wa binadamu mwenzio. Zama hizi watu wamepumbazwa na kujazwa ujinga wa kumsahau Mungu ambaye ni kila kitu. Haiingii akilini eti ubongo wa jambazi unaweza kukupa utajiri,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Inadaiwa siku ya tukio majambazi hao walipanga kuvamia nyumba moja ya kulala wageni kwa nia ya kupora fedha kiasi cha shilingi milioni 20 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja aliyefikia hotelini hapo.

No comments:

Post a Comment