Tuesday, April 22, 2014

BADO TUNAYO NAFASI KUNUSURU KATIBA MPYA

NIANZE kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kila hatua ya maisha yangu, kwa sababu ninaamini kabisa, bila yeye, hakuna lolote ninaloweza kulifanya.
Nichukue nafasi hii pia kukusisitiza Mtanzania mwenzangu, ni vyema tukaanza kujiandaa mapema kwa ajili ya makazi yetu ya baadaye, ambayo ni kutenda mema yanayompendeza Mungu, kwa imani uliyonayo, kwa sababu kuna maisha baada ya kifo.
Aidha, niwape pia mkono wa Pasaka waumini wote wa dini ya Kikristo, wakati huu wanapokumbuka siku ya kifo cha Bwana Yesu Kristo, kilichotokea zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Baada ya kutoa machache hayo, sasa turudi kwenye mada yetu ya leo.
Bunge Maalum la Katiba linaendelea na vikao vyake mjini Dodoma leo, lakini likiwa limepata mtikisiko mkubwa kufuatia kususa kwa baadhi ya wajumbe wake, wakiongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakitoa madai mbalimbali, yakiwemo ya kudharauliwa, kutukanwa na kutothaminiwa.
Kuondoka kwa wajumbe hao, ambao wengi ni kutoka vyama vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, kumewafanya wananchi kushindwa kuelewa nini hatima ya mjadala huo muhimu kabisa kwa nchi yetu, kwani sasa unaonekana kama utajadiliwa na upande mmoja tu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) au kama wanavyojiita bungeni, walio wengi.
Lazima niwe mkweli kwamba nimesikitishwa sana na kitendo kilichotokea huko Dodoma kwa sababu kina madhara makubwa sana kwa nchi yetu. Mjadala huu, kwa namna ninavyofahamu, hauna mshindi, kwa sababu wote ni wajenzi wa nyumba moja, imara na yenye mshikamano, Tanzania.
Tunapotaka kuifanyia mema nchi yetu, ambayo imekuwa ya amani na utulivu kwa muda wote tokea tulipojitawala, ni jambo la msingi sana kuepuka mtu au kundi moja kutafuta ushindi, hasa kwa suala muhimu kama hili la mjadala wa katiba.
Katiba tunayoitafuta, ambayo imekuwa ni madai yetu kwa miaka mingi kutokana na iliyopo kuwa na upungufu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kwenda na wakati, siyo ya chama chochote cha siasa au kundi lolote, isipokuwa ni katiba ambayo itanufaisha makundi yote ya kijamii na kisiasa yaliyomo nchini.
Kama suala lenyewe ni nyeti namna hii, ni vipi baadhi ya watu wadhani kwamba wanaweza kushiriki tendo hili tukufu peke yao? Ni kwa nini tunadhani bila sisi mchakato huu ni batili?
Nadhani upo umuhimu wa wajumbe wote, kutoka pande zote, walio wengi na wachache yanayotuwakilisha bungeni, kufikiri tena na kuona umuhimu wa kazi iliyopo mbele yao. Kazi hii ni ngumu, yenye kuhitaji maridhiano ya pamoja.
Wanapaswa kujua kwamba wakati wa mjadala wa rasimu hii, watu wote hatuwezi kufanana mawazo na ni kitu kibaya mtu au kundi moja kulazimisha matakwa yake pekee ndiyo yafanyiwe kazi. Tukubali kutofautiana, kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.
Tunaweza tukadhani kwamba tunachokifanya leo ni kwa sababu ya kizazi chetu pekee, kama ni hivi tutakuwa tunajidanganya sana. Katiba hii ni muongozo ambao utakuwa ndiyo dira ya taifa letu, huenda hadi vizazi vijavyo.
Kama tutafanya makosa leo, kwa kupitisha katiba yenye kukidhi matakwa yetu ya sasa, tunaweza kujikuta tukiwa sehemu ya watu wenye historia mbaya ya nchi yetu, kwa kuwa madhara yoyote yatakayotokea kufuatia uamuzi tunaoufanya sasa, hatuwezi kukwepa lawama.
Nitoe rai kwa wajumbe wa Bunge Maalum, wale wanaowakilisha Ukawa na CCM. Wananchi wanawategemea nyinyi kama ndiyo wawakilishi wao. Kupitia kwenu, wanaamini watapata rasimu iliyofanyiwa uchambuzi wa kina na wenye manufaa kwa taifa.
Tanzania ni zaidi ya muundo wa serikali. Kuna vitu vingi sana wanahitaji kuviona vikiwa ndani ya katiba hii, ili kupitia yenyewe, maisha yao yaweze kuboreshwa.
Mvutano unaoonekana hivi sasa, hauna maana kwao kwa sababu wanawaona wajumbe kama watu wanaopigania masilahi binafsi na vyama vyao badala ya taifa.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli. 

No comments:

Post a Comment