Thursday, April 10, 2014

JINSI YA KUANZA MAISHA YA KUJITEGEMEA-2

WIKI ya pili sasa nazungumzia mada ya jinsi ya kuanza maisha ya kujitegemea; ni imani yangu kuwa somo hili litawasaidia wengi. Pamoja na mambo mazuri niliyoandika wiki iliyopita, leo nakusudia kumalizia machache juu ya somo hili, ungana nami katika kutazama vipengele vilivyosalia.
KUJIAMINI
Vikwazo au shaka juu ya kuweza kumudu maisha ya kujitegemea vimewafanya wengi wasijiamini. “Kwa kipato hiki nitaweza kweli kuendesha maisha yangu, nilipe kodi ya nyumba, chakula, mavazi na mahitaji mengine?”
Maswali ya aina hii mara nyingi yamekuwa na majibu ya haitawezekana! Tabia ya akili hasa katika kufikiria mambo yajayo ni kujenga hofu ambayo wakati mwingine haihitajiki; wenye kujiamini pekee ndiyo ambao hutupilia mbali hofu na ndiyo waliofanikiwa katika maisha yao.
Kwa msingi huo, unapofikiria maisha ya kujitegemea usiwaze sana juu ya kuwezekana kwa mambo, jiamini kuwa utaweza, ukifanya hivyo utaweza; siku zote mwenye shaka havuki mto!
KUCHUKUA HATUA
Hatua nyingine muhimu baada ya kupita vipengele nilivyoanisha hapo juu ni hiki cha kuchukua hatua.
Watu wengi wamekuwa wakipanga kujitegemea, lakini kila mwaka wanaahirisha kufanya hivyo. “Nafikiri nitahamia chumba changu mwaka ujao.” Mwaka ukifika anapanga kufanya hivyo mwaka unaofuata matokeo yake anazeeka akiwa kwenye maisha tegemezi.
Ushauri wangu, baada ya kujiamini kuwa unaweza chukua hatua ya kutoka mahali ulipo, jambo kubwa la kuzingatia hapa ni kuhakikisha kuwa uchukuaji hatua lazima uambatane na ushauri mzuri kutoka kwa ndugu, na jamaa hasa wale uliokuwa unaishi nao kama wanakuunga mkono katika suala hilo.
KUTORUDI NYUMA
Uchunguzi unaonesha kuwa wapo watu ambao hupitia hatua zote za kuelekea kujitegemea, lakini wanapozikabili changamoto za maisha hayo huamua kurudi mahali wapokuwa wanaishi awali jambo ambalo huwaongezea fedheha na mara nyingine kuwaathiri kisaikolojia.
Unapokuwa umeanza maisha ya kujitegemea, suala la kurudi ulipotoka lisiwe la kawaida. Kumbuka unapokuwa na wazo la “nikishindwa narudi kwa baba,” huwezi kujituma, hutapambana na changamoto za maisha binafsi kwa vile kinga yako haitakuwa kwako bali kule ulikotoka, kushindwa itakuwa ni sehemu yako.
ONGEZA MARAFIKI
Unapokuwa kwenye maisha ya kujitegemea hakikisha kuwa unajitahidi kupunguza maadui. Fanya kila linalowezekana kuongeza marafiki ambao siku zote ndiyo nguzo muhimu nyakati za shida.
Kumbuka kazi ya rafiki ni kufariji na adui kuangamiza! Baada ya kusema hayo, naamini mada hii itawasaidia wengi, furaha yangu ni kusikia baada miezi, miaka michache kuwa watu wengi walijitegemea kutokana na hamasa waliyoipata kwenye soma hili! Asante kwa kuwa nami kwa wiki ya pili.

No comments:

Post a Comment