

Utajifunza kila siku na utavuna mengi uliyoyakosa kwa muda mrefu kabla ya kujiunga nasi. Sasa turejee kwenye somo letu ambalo leo linafikia ukingoni.
Tunajifunza kuhusu mateso katika mapenzi. Nimeshafafanua mengi katika matoleo mawili yaliyotangulia lakini kubwa zaidi ambalo nimesisitiza ni kwamba, mapenzi hayatakiwi kukutesa hata kidogo.
MATESO YA KUJITAKIA
Inaweza kukushangaza kidogo, lakini nakuambia rafiki yangu, wakati mwingine unaweza kusababisha mateso katika maisha yako mwenyewe. Mateso hayo, utayasababisha kwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na utaratibu kwa mpenzi wako.
Wapo baadhi ya watu huamua kufanya makosa kwa makusudi wakiamini kwamba hawawezi kuachwa kwa sababu wapenzi wao wanawapenda sana! Huko nakuita ni uvivu wa kufikiri.
Kamwe usiwe mvivu wa kufikiri mambo, unaweza kumfanyia visa leo, ukamtesa na kumnyanyasa, lakini ipo siku moyo wake utachoshwa na mambo yako, utachoshwa na mateso na mwishowe unaweza kuachwa kwenye mataa.
Kamwe usiwe mvivu wa kufikiri mambo, unaweza kumfanyia visa leo, ukamtesa na kumnyanyasa, lakini ipo siku moyo wake utachoshwa na mambo yako, utachoshwa na mateso na mwishowe unaweza kuachwa kwenye mataa.
Kama upo katika uhusiano na mpenzi wako ni vyema ukaonesha mapenzi yako, uoneshe jinsi unavyompenda. Jinsi unavyojali ili penzi lenu lizidi kukua siku hadi siku.
Upo mfano wa wazi kabisa wa kijana mmoja ambaye alikuwa na mpenzi wake aliyempenda kwa miaka kumi kwenye mapenzi. Kila wakati mwanamke huyo alikuwa akimfanyia jamaa visa, kila siku visa vinazidi. Leo akifanya hivi, kesho anafanya vile.
Lakini kwa sababu jamaa alikuwa akimpenda sana mpenzi wake alikuwa akimvumilia. Hakuthubutu kumuacha, lakini ilifika wakati akaona hana sababu ya kuendelea kubaki na maumivu, akafanya uamuzi ambao ulimuumiza sana yule mchumba wake. Ulimuumiza kwa sababu haukuwa mzuri.

Kama ni kweli unahitaji furaha katika maisha yako ya kimapenzi, badilika. Chunguza mapito yako, angalia wapi unapokosea kisha anza upya ili furaha iwe sehemu ya maisha yako.
JIFUNZE KUTOKA KWA MWENZAKO
Si vibaya kuwa mwanafunzi kila siku. Usikubali kuwa mtu wa kulia kila wakati. Ni vyema pia kujifunza kutoka kwa mwenzako.
Angalia anapenda nini na anachukizwa na jambo gani? Kuyajua kutakusaidia sana kukwepa yale mabaya ambayo hayafurahii kisha utafanya mazuri ambayo yatasaidia zaidi kukuza uhusiano wenu.
Mapenzi ni furaha ndugu zangu, hakuna tatizo kuwa mjinga kwa muda ili utengeneze kitu kizuri na kikubwa kwenye uhusiano wako. Kuna sababu gani ya kuishi bila amani?
Mapenzi ni furaha ndugu zangu, hakuna tatizo kuwa mjinga kwa muda ili utengeneze kitu kizuri na kikubwa kwenye uhusiano wako. Kuna sababu gani ya kuishi bila amani?
Kwa nini uumizwe na amani ya wengine? Maana inawezekana wewe na mwenzi wako kila siku ugomvi lakini nyumba ya pili wanaishi kwa amani na upendo.
Unawaona wanapita wakiwa wenye nyuso za furaha siku zote. Hakuna jipya, ni kutengeneza uhusiano wenye nguvu, ushirikiano, kusikilizana na upendo wa dhati.
Huna sababu ya kutoa machozi yako tena kwa ajili ya mapenzi. Mada imeisha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
No comments:
Post a Comment