Wednesday, July 25, 2012


Kada CCM jela miaka 18 kwa wizi wa EPA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miaka 18 jela Kada wa CCM, Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala Hussein katika kesi ya tuhuma za kuchota Sh2.2 bilioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mahakimu wawili katika jopo la waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo waliwatia hatiani watuhumiwa kwa makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.

Kwa upande wake kiongozi wa jopo hilo, Jaji Fatuma Masengi aliwaachia huru washtakiwa hao kwa maelezo kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka yote saba yaliyokuwa yanawakabili.

Hata hivyo, hukumu hiyo haikuweza kuwaokoa watuhumiwa na hasa Farijala na Maranda watatumikia adhabu yao kwa miaka mitatu jela kwa kuwa adhabu zote walizopewa zitakwenda kwa wakati mmoja.

Tayari Maranda na Farijala wanatumikia kifungo kingine cha miaka mitano jela, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.8 bilioni za EPA, ambapo walihukumiwa na mahakama hiyo Mei 23, 2011.

Jopo lagawanyika
Jopo la mahakimu watatu lililokuwa likisoma hukumu hiyo liligawanyika na kusoma hukumu mbili tofauti, ambapo hukumu moja iliyoandaliwa na kusomwa na kiongozi wa jopo hilo, Jaji Masengi aliyewaachia huru washtakiwa.

Hata hivyo, katika hukumu ya pili, iliyoandaliwa na Hakimu Projestus Kahyoza na mwenzake Catherine Revocate iliwatia hatiani washtakiwa katika makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili, na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa.

Hata hivyo, wakati wakisoma hukumu hiyo, mahakimu hao walisema badala ya washtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 18, hukumu yao itaenda sambamba hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Kabla ya hukumu
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, hakimu Kahyoza na mwenzake walipitia ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa  mashtaka  akiwamo mtaalamu wa maandishi, Joseph Mgendi ambaye aliweza kuangalia saini katika nyaraka halisi na zinazodaiwa kughushiwa,  ikiwamo hati ya usajili  ambapo alibainisha kuwa zilikuwa zimeghushiwa.

Pia walipitia utetezi uliotolewa wa mshtakiwa Maranda, ambaye aliyakana mashtaka yote saba yanayowakabili na kwamba, alikataa katakata kuwa hakuwahi kula njama na kughushi hati ya usajili wa Kampuni ya Money Planners & Consultant.

Hakimu Kahyoza alisema, Maranda alidai kuwa yeye hakuwahi kwenda Brela kusajili kampuni hiyo na kwamba, aliyewahi kwenda kusajili kampuni ni binamu yake, Farijala.

Hakimu Kahyoza alisema, Maranda katika utetezi wake alisema yeye hakuwahi kughushi hati yoyote hivyo, haikuwa rahisi kwake kutoa hati iliyoghushiwa pia, hakuwahi kuiba fedha BoT na wala hakuwahi kujipatia fedha yoyote kwa njia ya udanganyifu.

No comments:

Post a Comment