
Na Khadija Mngwai
KLABU ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam, imesema imedhamiria kuvunja mwiko Kanda ya Ziwa kutokana kwa kuhakikisha inapata ushindi wa pili katika kanda hiyo.
Azam iliifunga Kagera Sugar bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara na inataka kuifunga Toto African kwenye mechi ya pili itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ili ivune pointi sita Kanda ya ziwa.
Azam haijawahi kuvuna pointi hizo kwenye kanda hiyo tangu ilipopanda daraja miaka mitano iliyopita.
Akizungumza na Championi Jumatano, msemaji wa timu hiyo, Jaffer Idd, alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanashinda mchezo huo dhidi ya Toto ili waweze kujihakikishia pointi tatu muhimu na kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi.
“Maandalizi yanaendelea vizuri kama tulivyopanga, timu iliondoka Bukoba Jumapili saa 9:00 kwa ndege na kutua Mwanza saa 10:00 ambapo kikosi kilipumzika na kuanza mazoezi leo Jumatatu na Jumanne na tupo tayari kuikabili Toto.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunaifunga Toto ili tuweze kuvunja mwiko uliokuwepo Kanda ya Ziwa kutokana na kutoshinda mara kwa mara, hivyo tunahitaji kufungua ukurasa mpya.
“Kwa upande wake, kocha wetu (Boris Bunjak) amefurahishwa na matokeo hayo kwa kuwa alikuwa hajui kama hatujawahi kuifunga Kagera nyumbani kwao tangu tuingie kwenye ligi misimu kadhaa iliyopita, hivyo amesema ni mwanzo mwema kwake na amekipanga kikosi chake kuhakikisha kinashinda katika kila mechi,” alisema Jaffer.
Alisema kikosi chote kipo fiti na wachezaji wanaonyesha kiwango kizuri na hakuna majeruhi hata mmoja na kudai kuwa wameondoka na kikosi pungufu kutokana na kuepuka gharama kwa kuwa wasingeweza kusafiri na wachezaji wote.
No comments:
Post a Comment