Thursday, September 13, 2012

MAAMUZI YA KAMATI YA UTENDAJI YA SIMBA, GAZETI LA NIPASHE


KUFUATIA maamuzi ya kikao cha Kamati ya Katiba na Sheria ya TFF kilichokaa Jumatatu iliyopita kujadili hatma ya wachezaji Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, Kamati ya Utendaji ya Simba SC ilikutana kwa siku mbili mfululizo (Septemba 11 na 12) kujadili kuhusu maamuzi hayo.
Kabla ya kutangaza maamuzi ya Kamati ya Utendaji, nitumie nafasi hii kuwashukuru wanachama waandamizi wa klabu; Mzee Samuel Sitta, Profesa Philemon Sarungi, Mzee Yusuf Makamba na Profesa Juma Kapuya kwa mchango wao mkubwa wa kimawazo kwa kamati ya utendaji ambao ulikuwa na ushawishi mkubwa kwenye kufikia maamuzi ambayo tumeyafikia.
Kamati ya Utendaji ya Simba imefikia maamuzi yafuatayo.
  1. Simba haitajitoa kushiriki katika michuano yote inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Ingawa uongozi ulipata shinikizo kubwa kutoka kwa wapenzi na wanachama wake la kutaka timu ijitoe kwa kutoridhishwa na maamuzi ya kamati ya sheria, uongozi umeona ni vema timu ikashiriki ligi. Uamuzi huu umezingatia ukweli kwamba kujiondoa kwenye ligi usingekuwa uamuzi wa kimichezo. Hivyo Simba itashiriki katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu unaoanza wikiendi hii.
  1. Kwamba wanachama au wapenzi wote waliokuwa na nia ya kutaka kupeleka suala hili mahakamani wasitishe dhamira yao hiyo. Iwapo suala hili litapelekwa mahakamani, klabu inaweza kuathirika kwa namna nyingi ikiwamo kuzuiwa kushiriki mashindano yoyote yanayotambuliwa na TFF, CAF na FIFA.
  2. Kwamba uongozi wa Simba unaendelea na jitihada nyingine za kutafuta haki kwenye maamuzi hayo ya kamati.
  3. Uongozi unalipeleka kwenye vyombo vya dola suala la mchezaji Kelvin Yondani. Kwavile mchezaji mwenyewe amekataa kuwa hakusaini Simba, namna pekee ya kumaliza utata kwenye hili ni kulipeleka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vina vifaa na watu wenye uwezo wa kung’amua alama za vidole za watu.
  4. Uongozi wa Simba utakuwa ukitoa taarifa za mara kwa mara kila zinapokuja kuhusiana na masuala haya na unawataka wanachama na wapenzi wake kutulia wakati uongozi ukiendelea kuyashughulikia 
Gazeti la NIPASHE
KATIKA gazeti la NIPASHE toleo la leo Septemba 13, 2012, ukurasa wa mwisho kuna habari yenye kichwa cha habari; “Rage Bingwa wa Kudanganya.”
Habari hiyo ndiyo ilikuwa habari kiongozi (lead story) ya gazeti hilo kubwa na la kuheshimika hapa nchini.
Ndani ya habari hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, ameelezwa kuwa ni mtu mwongo na anayependa kudanganya watu kila wakati.
Habari hizi zimemsikitisha Rage binafsi na kumfedheesha kila mwenye kuitakia mema Simba.
Kinyume kabisa cha misingi ya taaluma ya uandishi, habari hiyo ya NIPASHE imeandikwa pasipo kumhoji Rage mwenyewe au kiongozi yeyote wa Simba. Simba ingeelewa kama mwandishi angeandika taarifa ile kama wazo binafsi au makala.
Lakini kuiandika kama habari, kwa kunukuu taarifa za upande mmoja na zenye lengo la kutaka kumdhalilisha Mwenyekiti na klabu ya Simba, gazeti la NIPASHE limekwenda mbali sana.
Kwa mfano, gazeti hilo limeeleza “uongo” mmojawapo wa Rage kuwa ni hatua yake ya kutangaza kuitisha Mkutano Mkuu wa wanachama baada ya maamuzi ya Kamati ya Mgongolwa.
Gazeti hilo limedai kwamba huo ni uongo kwa vile ili kuitisha mkutano, Mwenyekiti anahitaji idhini ya zaidi ya theluthi mbili ya wanachama. ! Hata hivyo, Katiba ya Simba inampa Mwenyekiti ridhaa ya kuitisha Mkutano Mkuu wa dharura wakati wowote atakapoona inafaa.
Suala la theluthi mbili linakuja wakati wanachama wanapotaka kuitisha mkutano huo wakati uongozi ukiwa hautaki. Lakini huu umeelezwa pia kama “uongo” wa Rage.
Ikumbukwe pia kwamba Mheshimiwa Rage ni mbunge, mwenyekiti wa Simba na ni mtu ambaye amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali katika sehemu nyeti.
Kusema kwamba mtu wa namna hii ni bingwa wa kudanganya ni matusi kwa watu wanaomchagua kushika nafasi za heshima na wale waliowahi kumteua kushika nafasi hizo kwa kuzingatia uchapakazi wake, ushawishi wake na mvuto alionao kwa wananchi.
Simba haina nia, sababu wala haja ya kugombana na chombo chochote cha habari achilia mbali NIPASHE. Hata hivyo, kwa sababu taarifa hii imegusa hadhi ya mtu binafsi na taasisi anayoiongoza au watu wanaomwamini, klabu ingeomba yafuatayo kutoka gazeti la NIPASHE.
Kwanza, gazeti hilo liombe radhi katika kipindi cha siku saba kutoka leo kuhusiana na habari hizo ambazo zimemsononesha sana.
Pili, radhi hiyo iombwe kwa ukubwa uleule ambao habari ya leo iliandikwa.
Kinyume cha hayo, Rage na Simba haitasita kutafuta njia nyingine ya kusafisha jina na hadhi yake binafsi na hadhi ya wale ambao wanamheshimu.

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

No comments:

Post a Comment