Kikosi cha Yanga kilichoilaza African Lyon mabao 3-1 jana.
Na Khatimu Naheka
IKICHEZA mchezo wake wa nne katika Ligi Kuu Bara, Yanga imefanikiwa kukwea mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo, baada ya kuifunga African Lyon mabao 3-1 katika mchezo mkali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya timu hiyo ibakize pointi tano kuwafikia mahasimu wao, Simba, waliopo kileleni, kuelekea kwenye mtanange kati ya timu hizo utakaochezwa keshokutwa kwenye uwanja huo.
Yanga jana ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyefunga katika dakika ya 16, akiunganisha kwa ustadi krosi aliyopewa na Haruna Niyonzima.
Pamoja na Yanga kutawala mchezo huo kwa muda mrefu, ilijikuta ikifedheheshwa katika dakika ya 63, baada ya makosa ya beki Oscar Joshua kuzembea kuokoa mpira ndani ya eneo la hatari, kumfanya Jacob Masawe aisawazishie timu yake, lakini Lyon wakiwa wameduwazwa na furaha ya bao, walijikuta wakipigwa bao la pili dakika moja baadaye, likifungwa na Nizar Khalfan aliyepata krosi safi kutoka kwa Simon Msuva.
Baada ya bao hilo, Yanga ndiyo walioendelea kutawala mchezo, hatimaye Nizar akafunga bao la tatu katika dakika ya 89 na kuhitimisha ndoto za Lyon kusawazisha. Nizar aliyetemwa na Klabu ya Philadelphia Union ya Marekani, amefungua akaunti yake ya mabao kwenye ligi hiyo kwa kishindo, kufuatia mabao hayo.
Huu ni mchezo wa mwisho kabla Yanga haijavaana na Simba kesho kwenye Uwanja wa Taifa.
No comments:
Post a Comment