Saturday, December 22, 2012

ROSE MUHANDO ABANWA KUTOKA NA MSANII WAKE, AFUNGUKA


Stori: George Kayala
MALKIA  wa muziki wa Injili nchini, Rose Salum Muhando juzikati aliifungukia ishu ya kudaiwa kutoka kimahaba na mpiga kinanda wake  anayejulikana kwa jina moja la Yusuf na kudaiwa kumtimizia kila anachokihitaji kijana huyo ambaye ni mdogo kiumri kuliko yeye.

Akizungumza na ‘kachala’ wa Funguka na Risasi Jumamosi hivi karibuni jijini Dar, Rose alisema hata yeye  amekuwa akisikia maneno hayo kutoka kwa wabaya wake lakini hakuna ukweli wowote.
“Hakuna ukweli wowote juu ya suala hilo kwani hayo ni maneno ya watu ambao wanakusudia kuharibu huduma yangu. Siwezi kutembea na kijana huyo ambaye kwanza ni sawa na mdogo wangu wa pili,” alisema Rose.
Funguka: “Lakini Rose lisemwalo lipo kama halipo linakuja, yawezekana kukawa na ukweli juu ya suala hili, naomba uwe mkweli.”
Rose: “Hapana, mimi ni mtumishi wa Mungu siwezi kusema uongo. Unajua mimi sijaolewa hivyo watu wakiona nipo karibu na mwanaume yeyote wanaaminisha akili zao kwamba nina uhusiano naye wa kimapenzi, kitu ambacho kwa kweli kimekuwa kikinikosesha amani kila ninaposikia.”
Funguka: “Rafiki zako wa karibu ndiyo wanaosema hivyo. Je, tusiwaamini?”
Rose: “Kumbuka kikulacho ki nguoni mwako. Wimbo wangu wa Nibebe nilioimba kwenye albamu yangu iliyopita naamini ukiusikiliza vizuri utakupa majibu ya nini nilichomaanisha juu ya marafiki zangu.
“Naamini kuwa si wote wana mapenzi mema na mimi, wapo wanaochukia maendeleo yangu na wengine wananiombea mazuri.
“Ni kweli Yusuf ni mpiga kinanda wangu na nimekuwa karibu naye sana kwa masuala ya kazi kwani hii ndiyo ajira yangu. 
“Sina kazi nyingine zaidi ya hii, hivyo ni vizuri kuwa karibu na watu. Nikifanya hivyo kwa wanaume naonekana natoka nao kimahaba, mbona hawasemi kwa wanawake?”
Funguka: “Kwa nini usiolewe ili uondokane na skendo za kuzushiwa  kutoka kimahaba na watu unaofanya nao kazi?”
Rose: “Kila jambo lina wakati wake. Majira yakifika Mungu atanipa mume wangu ambaye ataipenda huduma yangu pia, kwani ninaweza kuolewa na mwanaume mwenye wivu na kuua huduma ya uimbaji ambayo imenifikisha hapa nilipo.”
Funguka: “Ina maana mpaka sasa hujaona mwanaume mwenye sifa ya kukuoa? Maana na umri nao unakwenda mbio.”
Rose: “Siwezi kusema chochote kwa sasa lakini ikimpendeza Mungu mwaka 2013 hautapita kabla sijaolewa.” 
Funguka: “Ina maana tayari umeshampata mchumba?”
Rose: “Nasema usiwe na haraka ya kujua suala hilo wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi kwani suala la kuolewa ni jambo la kheri, siwezi kulifanya kwa kificho. ”
Funguka: “Inasemakana hivi karibuni ulichumbiwa na mwanaume mmoja wa Mwanza ambaye ulimpenda kwa moyo wako wa dhati lakini mliachana baada ya kubaini kuwa jamaa alikuwa na mke na watoto. Je, ni kweli?”
Rose: “Si kweli, mimi sijawahi kuchumbiwa na siku ikitokea ikawa hivyo nitautangazia umma wa Watanzania ili kila mmoja ajue. 
Funguka: “Vipi kuhusu meneja wako Nathan, nasikia mmeachana naye na sasa unasaka meneja mwingine.”
Rose: “Siwezi kusema chochote juu ya Nathan ninachojua mimi bado nafanya naye kazi.”
Funguka: “Kwani kuna ugumu gani wewe kuniambia ukweli wa suala hilo?”
Rose: “Nimesema siwezi kusema chochote, kama maswali yameisha naomba uniache niendelee na mazoezi ya kuimba.”
Funguka: “Nikutakie kazi njema Rose.”
Rose: “Asante karibu wakati mwingine.” 

No comments:

Post a Comment