Saturday, March 9, 2013

USIPOJIANGALIA IPO SIKU UTAMPA PENZI KICHAA ILI AKURIDHISHE FARAGHA!


Leo nataka kuzungumzia hili suala la baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakiziendekeza tamaa zao kwa wanaume wengine na kujikuta wakiharibu ndoa na uhusiano wao.
Katika hili, unakuta mwanamke yuko ndani ya ndoa na mumewe anampenda na anajitahidi kumtimizia kila kitu lakini cha ajabu mwanamke huyo anaweza kusaliti eti kwa kuwa hapewi raha aliyoitarajia kwa mumewe pale wanapokuwa faragha.
Naandika haya kwa kuwa kuna tukio la juzi tu lililomtokea rafiki yangu. Jamaa huyu alikuwa na mke wake na kwa kuwa mwanaume alikuwa mchakarikaji, amekuwa akijitahidi sana kumpatiliza mkewe kwa kila kitu.
Katika kufanya hivyo mwanaume huyo amekuwa akijisahau hata katika kuvaa vizuri ili kuhakikisha mkewe anavaa na kupendeza. Maskini kumbe mke alikuwa analo linalomkosesha amani. Eti mumewe huyo alikuwa haiwezi kazi pale wanapokuwa kwenye uwanja wa kujidai!
Matokeo yake sasa, licha ya mwanaume huyo kujitahidi kwa hali na mali kumtimizia mkewe lakini kwa hili la faragha imekuwa sababu ya mwanamke huyo kutafuta kivulana nje ya ndoa.
Kinachouma zaidi mvulana huyo aliyepewa nafasi ya kumtimizia mke wa mtu huyo hana mbele wala nyuma. Sasa ilimuumaje siku ambayo mume alikuja kubaini kuwa anasalitiwa?
Kwa kifupi rafiki yangu huyo aliumia sana, aliona kumbe aliyokuwa akimfanyia mkewe yote yalikuwa bure eti kwa kuwa tu faragha kulikuwa na kasoro. Hata kama hilo ni tatizo, kwa nini huyu mke asiliweke wazi kwa mumewe ili wajue namna ya kulitafutia ufumbuzi?
Ni sahihi kweli kumsaliti mwenza wako eti kwa kuwa unapokuwa naye faragha hakufikishi? Mimi nadhani ifike wakati tuache hizi tamaa za kijinga.
Kama wewe umeingia kwenye ndoa na umebahatika kumpata mume anayekupenda na kukutimizia shida zako, nawe mpende na mheshimu.
Kama umeona upungufu kwake, jadilianeni mjue jinsi ya kukabiliana nao. Tambua huenda na wewe pia una udhaifu wako na anakuvumilia.
Naomba niseme kwamba, tuache tamaa za kijinga za kuwasaliti wapenzi wetu kwa sababu ya kuwepo kwa upungufu unaoweza kuvumilika. Hivi unachukuliaje pale ambapo mumeo anakununulia vitu vya gharama kwa kuwa anakupenda kisha wewe unavivaa na kwenda kumsaliti kwa mwanaume ambaye wala hana mpango na wewe?
Unajichukuliaje pale unapochukua fedha ambazo amekuachia mumeo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kisha kumhonga kijana ili tu akufurahishe kimapenzi?  Huoni huko ni kujidhalilisha?
Mumeo anapokuwa  na upungufu wewe ndiye unayetakiwa kuwa mstari wa mbele kukabiliana nao. Mpe moyo, ongea naye, mpe mbinu nyingine mnazoweza kuzitumia ili muwapo faragha mfurahi wote.
Tusisalitiane kwa sababu ya upungufu wetu, tutambue kuwa kila mmoja hajakamilika hivyo kuvumiliana ndiyo silaha ya pekee inayoweza kuzidumisha ndoa na uhusiano wetu.
Mwisho naomba kusema kwamba, heshima yako ni muhimu sana kuliko chochote. Kama umejaaliwa kuingia kwenye ndoa, tulia kwani ndoa ni heshima. Usiuze utu wako kwa bei chee. Kumbuka wapo waliojaaliwa kuolewa na wanaume wanaojua mapenzi kweli lakini hawazitamani ndoa zao kwa kuwa waume zao hawaoneshi kuwapenda na kuwajali.
Sasa jiulize, kipi bora kuolewa na mwanaume ambaye anakupenda, anakujali, anakuthamini na kukuheshimu lakini ana tatizo kidogo pale unapokuwa naye faragha au kuolewa na yule ambaye shughuli anaijua kweli lakini haoneshi kukupenda kwa dhati, hakujali na wala hakuheshimu?
Jibu unalo na nikuambie tu kuwa, usipojiangalia kwa tamaa yako ipo siku utatembea na kichaa eti ili tu akuridhishe faragha.

Tukutane wiki ijayo. 

No comments:

Post a Comment