Friday, September 28, 2012

Mgosi: Naifunga Simba leo


Mussa Hassan Mgosi.
Na Khadija Mngwai
MSHAMBULIAJI wa JKT Ruvu, Mussa Hassan Mgosi, amesema wanahitaji kupata pointi tatu kutoka kwa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mgosi anahitaji ushindi wa pili mfululizo baada ya awali kikosi chake kufanikiwa kuifumua Ruvu Shooting mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mgosi, ambaye alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2009/10 akiwa na kikosi cha Simba, alisema mechi yao dhidi ya Wekundu hao itakuwa ngumu kutokana na kila timu kujiandaa vya kutosha.
“Siihofii Simba, cha muhimu kwetu ni kuhakikisha tunaibuka na pointi tatu kutoka kwao, kwani tunasubiri dakika 90 ndizo zitasema kila kitu, tumejiandaa vizuri na wachezaji wote wapo katika kiwango kinachotakiwa.
“Nimejipanga vyema kuikabili Simba kwa kuhakikisha naifunga, nipo vizuri na nimeelewana vyema na wachezaji wenzangu kwa kuwa Ruvu ndiyo timu yangu iliyonikuza, hivyo nimeweza kuzoeana nao haraka,” alisema Mgosi.
Alisema wanajua watakutana na ushindani wa hali ya juu katika mchezo huo lakini hawatakubali kuipa nafasi timu hiyo kuweza kuwafunga kirahisi na wanachokitaka wao ni pointi tatu kutoka kwa Simba.
Simba iliifumua African Lyon mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar. JKT wenyewe walifanikiwa kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment