Friday, September 28, 2012

The Rotten Deal (Mpango Ulioharibika) - 32


LICHA ya kutumia nguvu kubwa kuficha sababu ya kifo cha mumewe, Barbara Washington anafanya makosa mara kwa mara yanayozidi kumuweka katika sehemu mbaya ya kugundulika kuwa yeye ndiye aliyekuwa nyuma ya mauaji ya watu kadhaa kwa lengo la kuficha aibu ya mumewe kutumia madawa ya kulevya.
Uzembe mkubwa unafanyika wakati wa kumteka askari aliyekuwa miongoni mwa walinzi wa makazi ya Barbara, Shakoor ambapo baada ya kumteka na kwenda kumuua kisha kumteketeza kwa moto ndani ya msitu wa Kanyovu, wanasahau kuichukua simu yake iliyodondoka eneo walipomteka.
Majasusi wa KGB nao wanaongeza kasi ya kupeleleza ukweli juu ya tukio la kifo cha aliyekuwa rais wa Buzilayombo, Tony William, baada ya kugundua kuwa kuna watu wanawawinda ili wawatoe roho kwa lengo la kuficha ukweli juu ya kifo hicho na sasa wanamfuata Barbara na kumhoji ili kupata ukweli.
Je, nini kinafuatia? SONGA NAYO…
MUDA mfupi baada ya majasusi wa KGB kufika hospitali kumjulia hali mwenzao, Nestory aliyekuwa anauguza jeraha la risasi aliyopigwa mguuni ndani ya hoteli, walipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama mlinzi wa nyumba aliyokuwa anaishi Barbara Washington, mjane wa rais Tony William.
Mtu huyo aliwaambia kuwa anataka kuonana nao ana kwa ana kwa sababu kuna jambo muhimu ameligundua kuhusu Barbara, akawataka wafanye haraka kurudi na kuonana naye.
“Nimesema njooni haraka, mtanikuta barabarani nawasubiri, kuna siri nzito nimeigundua muda huuhuu, nataka kuongea nanyi ana kwa ana,” alisikika mtu yule aliyejitambulisha kuwa anaitwa Afande Shakoor.
“Sawa tunakuja sasa hivi,” alijibu Brian, akawageukia wenzake na kuwaeleza alichoambiwa.
“Anaongea huku akihema kwa nguvu mithili ya mtu anayekimbia, inawezekana kuna tatizo kubwa,” alisema Brian, wote wakahisi hivyo na kukubaliana kurudi nyumbani kwa Barbara haraka iwezekanavyo.
Brian na Elly walitoka na kumuacha mwenzao akiendelea kupatiwa matibabu, wakaenda mpaka sehemu walipokuwa wamepaki gari lao, wakaingia na bila kupoteza muda, safari ya kuelekea nyumbani kwa Barbara ikaanza. Wakawa wanakatiza mitaa ya Chato kwa spidi kubwa kuwahi eneo walilokubaliana kukutana na yule mlinzi.
Upande wa pili, baada ya Barbara kuona hatari iliyokuwa mbele yao endapo simu ile itaokotwa na mtu mwingine, harakaharaka alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia Zebedayo, akamwambia aingie ndani kwani alikuwa na mazungumzo nyeti.
Bila kupoteza muda, Zebedayo aliingia bila kuonekana na mtu yeyote, Barbara akatoka chumbani na kwenda kukaa naye sebuleni.
“Inatakiwa utoke sasa hivi na kwenda pale tulipomteka Shakoor, hakikisha simu yake inapatikana haraka iwezekanavyo kabla haijaokotwa na watu wengine. Ukichelewa unajua madhara yatakayotukuta… nenda sasa hivi,” alisema Barbara, Zebedayo akatoka mbiombio hadi nje.
Akamrubuni yule mlinzi wa getini na kufanikiwa kutoka, akaenda moja kwa moja mpaka eneo la tukio, akawa anajaribu kuangaza macho huku na kule bila mafanikio. Aliposhindwa kuiona, alitoa simu yake ya mkononi na kuanza kupiga ile namba ya Shakoor.
Kwa mbali akawa anasikia simu ikiita, akaendelea kuitafuta huku akisikiliza kwa makini mlio ulipokuwa unatokea. Akiwa bado anaendelea na kazi ile, alishtuka baada ya kuona gari la wale majasusi wa KGB likija kwa kasi kubwa pale alipokuwa anaendelea kuitafuta ile simu.
“Mungu wangu, nimekwisha,” alisema Zebedayo huku akijiuliza kama akimbie au asimame. Akiwa bado anajiuliza, lile gari lilikuwa tayari limeshawasili, dereva akafunga breki za ghafla pembeni ya Zebedayo ambaye bado alikuwa amejawa na kihoro akiwa haelewi kinachoendelea.
Harakaharaka wale majasusi wawili wa KGB waliteremka na kumfuata Zebedayo, wakaanza kumuuliza maswali ambayo yalizidi kumshangaza Zebedayo.
“Tumekuja, vipi una habari gani unayotaka kutuambia?”
“Habari? Mbona siwaelewi?”
“Kwani wewe si mlinzi wa Barbara Washington?”
“Ndiyo.”
“Wewe si ndiye uliyetupigia simu na kusema tukutane hapa?”
“Hapana, labda mmenifananisha.”
“Kwani wewe hapa unafanya nini?”
“Nimeangusha funguo ya nyumbani kwangu,” alisema Zebedayo.
“Tukusaidie kutafuta?”
“Hapana, nyie mnaweza kuendelea na kazi zenu,” alijibu Zebedayo huku akijifanya kuendelea kutafuta kile alichodai ni funguo. Wale majasusi wa KGB walitazamana huku wakionyesha dhahiri kushangazwa na Zebedayo, wakahisi kuwa huenda kuna jambo halikuwa sawa. Wakaingia ndani ya gari lao na kuendelea na safari ya kuelekea nyumbani kwa Barbara.
Kabla hawajawasha gari lao, waliamua kupiga namba ya simu ya Afande Shakoor na kumuuliza mahali alipokuwepo lakini cha ajabu, walisikia mlio wa simu ukisikika pembeni ya barabara, jirani na alipokuwa amesimama Zebedayo.
Wakateremka garini na kumfuata tena Zebedayo wakitaka kufahamu undani wa kilichokuwa kinaendelea.
“Hiyo simu inayoita ni ya nani?”
“Sijui. Mimi hapa ninachotafuta ni funguo, wala siyo simu,” alijibu Zebedayo huku akitetemeka, ikabidi wale majasusi waanze kuitafuta ile simu wao wenyewe. Muda mfupi baadaye wakafanikiwa kuipata, ikiwa kwenye majani marefu, pembeni ya barabara.
“Hii namba ndiyo iliyotutumia taarifa kuwa tuje hapa, sasa mwenyewe yupo wapi?”
“Mh! Huyu lazima atakuwa anaufahamu ukweli ila anataka kucheza na akili zetu.”
“Sifahamu chochote jamani wala hata hiyo simu simjui mwenye nayo,” alisema Zebedayo huku akizidi kutetemeka.
“Kinachokufanya utetemeke kiasi hicho ni nini?”
“Nani anatetemeka? Mimi ni mwanajeshi kamili siwezi kuzidiwa nguvu na hofu hata mara moja,” alisema Zebedayo huku akionyesha dhahiri kuchanganyikiwa kutokana na simu ile kutua mikononi mwa majasusi wale wa KGB.
“Tunahitaji kukuhoji kwa kina, ingia ndani ya gari twende mpaka nyumbani kwa Barbara,” alisema Elly lakini Zebedayo akawa mbishi, akasema atatembea kwa miguu. Ikabidi Brian aingie ndani ya gari na ile simu, Elly akawa anatembea na Zebedayo kurejea nyumbani kwa Barbara. 
Wakiwa wanaendelea kutembea, Zebedayo alitoa simu yake na kuandika ujumbe mfupi wa maandishi kwenda kwa Barbara akimtaarifu  juu ya kila kitu kilichotokea.
 ***
Mashirika makubwa ya ujasusi duniani, KGB la Urusi na CIA la Marekani, yalikuwa yakiendelea na kazi ya kufuatilia kwa kina sakata la kupatikana kwa fedha nyingi bandia katika mzunguko wa biashara nchini Buzilayombo.
Kiwango kikubwa cha fedha haramu kilichokutwa kwenye mzunguko, kiliilazimu Benki ya Dunia kuitisha mkutano wa dharura na viongozi wa mashirika hayo makubwa na yanayoaminika kwa upelelezi na ujasusi duniani na kuyapa kazi ya kufuatilia jinsi fedha hizo zilivyoingia kwenye mzunguko na watu wote waliokuwa nyuma ya tukio lile.
“Hatuwezi kusema tuzizuie zote kwa mkupuo kwani tutaua kabisa uchumi wa Buzilayombo, acha ziendelee kutumika lakini zile zote zitakazoingia kwenye mikono ya benki, itabidi zidhibitiwe zisitoke tena wakati uchunguzi ukiendelea.
 “Hii ndiyo sababu inayofanya nchi za Kiafrika kushindwa kuyafikia maendeleo ya kweli, lazima wahusika wapatikane haraka iwezekanavyo na kuchukuliwa hatua kali zitakazokuwa fundisho kwa wengine,” alisema Rais wa Benki ya Dunia wakati akizungumza na maofisa wa ngazi za juu wa mashirika hayo.
Je, nini kitafuatia? Usikose kwenye Championi Ijumaa.

No comments:

Post a Comment