Saturday, September 22, 2012

RAYMOND AND STEPHANIE (Raymond na Stephanie) - 15


BAADA ya kuhangaika kwa muda mrefu kuliita jina la mkewe bila kupata majibu, hatimaye David anakata tamaa na kuketi chini akiwa hajui cha kufanya. Akiwa katika  mawazo, ghafla anasikia sauti ya Catherine kwa mbali ikiomba msaada, hapo anatambua kwamba mkewe bado alikuwa ndani ya jumba hilo wanaloishi akiwa katika hali mbaya.
Anaifuatilia sauti na kumkuta  Catherine akiwa amelala chini na anapojaribu kumuita tena  hapati ushirikiano wowote kutokwa kwake,  David ananyanyuka na kukimbilia maji akiamini kwamba pengine yangeweza kumsaidia kwa kumfanya apate nguvu. Alichokifiria ndicho kilichotokea Catherine anapokunywa maji anapata fahamu lakini jambo jingine linajitokeza.
Catherine analalamikia maumivu  makali anayoyapata,  anamsisitiza mumewe afanye kila kinachowezekana kuhakikisha anampeleka anaokoa maisha yake.
Kichwa cha David kinawaka moto, anahisi mkewe ameshikwa na uchungu wa uzazi, hajui aanzie wapi kwani mpaka kufika hapo mkewe hajawahi kuhudhuria  kliniki hata siku moja.
 Huo unakuwa ni mtihani mzito kwake, anahofia maswali ya madaktari kuhusiana na maisha  yao.
Baada ya kuumiza kichwa kwa muda mrefu, uamuzi pekee ambao David anauchukua ni kutoka mpaka barabarani kutafuta usafiri ili kuweza kumpeleka hospitali mkewe, tayari alishakata shauri kuwa litakalokuwa na litokee, anakimbia kuelekea barabarani kutafuta usafiri bila ya kuhofia giza lililokuwa limetanda, imani yake anaitupa kwa Mungu akimuomba amsaidie ulinzi kwa mkewe na yeye pia.
“Ni lazima niyaokoe maisha ya mke wangu? siko tayari kushuhudia akifa na mtoto aliyeko tumboni apotee hivihivi,” David alitamka maneno hayo akikatiza vichaka kukimbilia barabarani.
Je, nini kitaendelea? Atafanikiwa kupata usafiri na kurejea na kumkuta mkewe akiwa  hai, atafanikiwa kumpeleka hospitali? je, kitu gani kitatokea huko? SONGA NAYO…

Mbali na giza lililokuwa limetanda usiku huo, baridi nalo lilikuwa kali kwelikweli lakini David alikuwa akivuja jasho mwili mzima.
 Alitembea kwa mwendo wa kasi pembezoni kabisa mwa barabara yenye vumbi huku akiendelea kumuomba Mungu amtendee muujiza wa kuweza kupata usafiri na kurejea kumsaidia mkewe.
“Mungu saidia, nitendee muujiza leo, nipate usafiri, nimpeleke mke wangu hospitali kwa jinsi anavyolalamika nahisi kabisa utakuwa ni uchungu,” David aliwaza huku akizidisha mwendo.
Kijasho chembamba kilikuwa kikimtiririka mwilini, hakika hakufahamu hatma ya maisha ya mkewe na mtoto wake mtarajiwa, ghafla akiwa katika dimbwi hilo la mawazo alisikia mlio wa pikipiki, awali hakuelewa ilikuwa ikitokea upande gani.
Alisimama na kuangaza kila upande, hatimaye akafahamu kuwa zilikuwa ilikuwa ikitoka nyuma yake kuelekea  kule alikokuwa akielekea.
Furaha ya ajabu ikaufunika moyo wake, akaamini kwamba Mungu ameyasikia maombi yake,  amefanikiwa alilokuwa akiliomba, akasogea pembeni kabisa mwa barabara ili kupata fursa nzuri ya  kuisubiri na kuisimamaisha pikipiki ile itakapofika usawa wake.
Jambo  la ajabu, David pamoja na kupungia mkono, alishangaa kuona  pikipiki ikimpita kwa kasi kama vile dereva alikuwa katika mashindano, akapigwa na butwaa, akachanganyikiwa kwani hakutegemea kilichotokea.
Ujasiri ukampungua moyoni mwake, akapiga ngumi hewani kulaani kitendo kile, akaona hakuwa na la kufanya zaidi ya  kusonga mbele.
Akiwa anajaribu kurudisha moyo wake wa kishujaa akasikia tena mlio mwingine wa pikipiki, safari hii  haikuwa pikipiki moja bali ni zaidi ya moja.
Akageuka kuziangalia na akazipungia mkono ili zisimame lakini ilikuwa  ni kazi bure, nazo zikampita kwa kasi.
“Mh! Mbona zinakimbia hivi halafu hazina hata abiria? Au pengine ni majambazi yanafukuzwa na polisi?”
Alibaki akiwa pembezoni mwa barabara akishuhudia pikipiki nyingine zikitokea na kumpita pamoja na jitihada zake za kuzisimamisha, madereva hawakusimama zaidi wengine  walimtukana.
“Mungu wangu ni kitu gani hiki? Kwa nini wananipita wakati wananiona na kusikia sauti yangu? Nahitaji kumsaidia Catherine mpaka sasa sijui kimetokea nini huko nyuma baada ya mimi kuondoka, masikini mke wangu…” aliongea kwa uchungu.
“Hapana ngoja nisimame katikati ya barabara pengine wataamua kusimama ili niwaeleze shida yangu wanisaidie.”
***
Hali ilizidi kuwa mbaya kadiri saa zilivyozidi kusonga, Catherine alikuwa amelala chini akigugumia kwa maumivu makali bila ya kuwa na msaada wowote, alijaribu kujivuta kwa nguvu  kutoka sehemu aliyokuwa ameketi lakini hakuweza kufanya hivyo. Maumivu makali yalikuwa yakimaliza jitihada zake.
 Mwili wake wote ulitota kwa jasho.
“Mh! Mh! Mungu wangu! Jamani, ninakuf…” alilalama Catherine ambaye joto lilikuwa limeutawala mwili wake.
“Lakini ngoja nijaribu kufanya kitu fulani angalau niweze kutoka nje kwenye upepo, pengine nitajisikia vizuri.”
Kwa muda wa dakika tano nzima Catherine aliendelea kujivuta kutoka sehemu aliyokuwa  amelala na hatimaye akafanikiwa kunyanyuka na kukamata ukuta na kuanza kutembea taratibu kuelekea nje.
“Nitakufa kabla David hajarejea, maumivu ni makali mno,” aliongea Catherine akiwa hapo akavisikia vitu vyepesi vikipenyeza kutoka katikati ya mapaja yake.
“Ni nini tena?” alijiuliza taratibu akaushusha mkono wake wa kushoto kugusa sehemu hizo lakini kabla hajafanikiwa  kufikisha mkono wake  kizunguzungu kikali kikamshika hatimaye giza zito likayafunika macho yake na kuanguka chini kama mzigo.
Uchungu mkali ulikuwa umemkamata na alichokisikia katikati ya mapaja yake kilikuwa ni damu iliyokuwa ikitiririka, dalili mbaya kabisa kwa mama mjamzito.
***
“Pikipiki nyingine hiyo inakuja, Mungu saidia mtu huyo asimame,” David aliongea akisogea katikati kabisa ya barabara bila kujali kitu.
Kama alivyofikiria baada ya pikipiki hilo kumkaribia huku dereva akionekana kukumbwa na wasiwasi akasikia sauti ya ukali ikimuuliza.
“Ni nani wewe na unafanya nini usiku huu mahali hapa?”
“Nisaidie ndugu yangu, okoa maisha ya mke wangu.”
“Mke wako?”
“Ndiyo, kafanya nini?”
“Ni mgojwa taabani na niko hapa kutafuta usafiri wa kumfikisha hospitali.”
“Mh,” dereva wa pikipiki aliguna.
“Tafadhali nisaidie nitakulipa fedha kidogo kama gharama ya usafiri wako.”
Kwa takribani dakika mbili nzima ukimya ukajitokeza kati yao huku pikipiki ikiendelea kuunguruma.
“Utanilipa shilingi ngapi braza?”
“Nitakupa tano tu ndugu yangu hali yangu si nzuri.”
“Ongeza kidogo nikusaidie.”
“Hiyo ndiyo niliyonayo hapa tafafhali kubali ndugu yangu.”
“Hebu geuka nyuma, nahitaji kukukagua pengine unaweza ukawa jambazi unataka kuniteka?”
“la hasha hiyo siyo nia yangu kwako.”
“Yuko wapi huyo mkeo?”
“Nyumbani lakini si mbali sana kutoka mahali hapa.”
“Haya panda twende nikusaidie.”
Dereva wa pikipiki alimuonesha ishara David kwamba azunguke na kupanda nyuma.

Je, nini kitaendelea? watamkuta Catherine akiwa mzima au amekufa? fuatilia Jumatano katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

No comments:

Post a Comment