


SAFARI za ndege zimerejea tena katika Jiji la New York, Marekani, japokuwa taratibu, na shughuli zingine za mambo ya soko la fedha zimerejea kwa kutegemea jenereta za umeme. Vilevile, pamoja na kwamba njia za treni za chini ya ardhi hazijatengemaa vyema, watu wengi walionekana wakitembea kuvuka Daraja la Brooklyn kuelekea sehemu ya Manhattan, jambo ambalo ni kinyume na ilivyokuwa wakati wa shambulio la kigaidi kwenye jiji hilo lililofanyika Septemba 11, 2001 ambapo watu wengi walikuwa wakikimbia kutoka Manhattan kuelekea Brooklyn.
Hayo yote yametokana na kimbunga kinachoitwa Superstorn Sandy ambacho kiliikumba sehemu ya kaskazini-mashariki mwa sehemu hiyo na kuua watu zaidi ya 70 juzi (Jumatano). Maeneo makubwa ya jiji hilo bado hayana umeme na shughuli zake nyingi zimesimama.
Sehemu kubwa ya wakazi wa jiji hilo, hadi habari hizi zinachapishwa, walikuwa wakihangaikia umeme, maji na huduma mbalimbali.
Gavana wa jiji hilo, Andrew Cuomo, alisema sehemu kadhaa za treni za chini ya ardhi zitaanza kufanya kazi leo, na kwamba njia tatu miongoni mwa saba za chini ya ardhi eneo la East River, zimenyonywa maji ili kuondoa vikwazo kabla ya kuanza huduma kamili.
Kwa kawaida, mabasi jijini New York huhudumia watu milioni 2.3 kwa wastani, lakini baada ya kimbunga hicho yalijikuta yakilazimika kuhudumia watu milioni 5.5 wakiwemo wale waliokuwa wakitumia treni za nchini ya ardhi.
Maeneo ya magharibi ya Wisconsin na Carolinas, kusini, kaya na biashara zaidi ya milioni sita zilikuwa hazina umeme, ikiwa nipamoja na kaya 650 jijini New York, alisema Meya Michael Bloomberg.
Meya huyo alisema wagonjwa 500 wamehamishwa kutoka Hospitali ya Bellevue kutokana na uharibifu wa kimbunga hicho na wagonjwa wengine 300 walihamishwa kutoka Hospitali ya Manhattan kutokana na ukosefu wa umeme.
Safari za ndege pia zimeanza katika viwanja vya Kennedy na Neward japokuwa kwa kiasi fulani, japokuwa uwanja wa LaGuardia bado haujaanza kupokea ndege kutokana na uharibifu uliotokea.
Vilevile, sehemu mbalimbali za jiji hilo, askari maalum walikuwa wakigawa vyakula vya kuliwa hapohapo vilivyokuwa katika magari mbalimbali, ambapo pia walikuwa wakishughulika na uokoaji wa watu kutoka katika majengo marefu.
CHANZO: LEADER-TELEGRAM
(Picha kwa hisani ya: AP, EPA, Reuters, Getty Images
No comments:
Post a Comment