Saturday, October 6, 2012

Waziri Chikawe chali CCM


MATOKEO yenye tafsiri ya mapinduzi ya kisiasa yameendelea kusikika katika uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), safari hii, Waziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ameangushwa na kijana mdogo mwenye umri wa miaka 24.
Waziri huyo, Mathias Chikawe anayeiongoza Wizara ya Katiba na Sheria, ameshindwa katika uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) katika wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.
Kuanguka kwa Chikawe kumethibitishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Lindi, Adelina Gefi alipozungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu.
Alisema nafasi ya Mjumbe wa NEC kutoka Nachingwea imekwenda kwa kijana mwenye umri wa miaka 24, Fadhili Liwaka aliyevuna kura 795 dhidi ya 561 alizopata Chikawe ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 61, huku mshindani mwingine katika nafasi hiyo, Lowama Mtonya (43) alipata kura 13 tu.
Hata hivyo, habari ambazo gazeti hili ilizipata zinasema kuwa, mshindi wa nafasi hiyo alikimbizwa hospitali mara baada ya matokeo, kutokana na kuanguka katika ukumbi wa mkutano na kupoteza fahamu jana jioni.
Amelazwa katika Hospitali ya Ndanda wilayani Masasi. Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, baada ya kuanguka na kuzimia kwa muda alizinduka na kumwambia baba yake mzazi, amwakilishe katika kuhesabu kura na yeye kukimbizwa hospitalini.
Wakati wengi wakipigwa butwaa na matokeo hayo, juzi wajumbe wa mkutano huo walimchagua Mkuu wa zamani wa wilaya, Albert Mnali kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM wilaya ya Nachingwea.
Mnali aliyejizolea umaarufu kutokana na msimamo wa kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wilayani Bukoba, mkoani Kagera kutokana na kile kilichodaiwa uzembe uliosababisha wanafunzi kufeli, msimamo uliomponza na kujikuta akivuliwa madaraka na kufukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete Februari 2009.
Katika uchaguzi wa juzi, Mnali ambaye mwaka 2010 alijaribu kuwania ubunge, lakini jina lake likaishia katika mchujo wa ndani ya chama, aliibuka mshindi wa nafasi ya uenyekiti baada ya kupata kura 948. Fadhili Mkuti alipata kura 251 na Mohammed Kamlo aliambulia kura 79.
Gefi aliongeza kuwa, katika uchaguzi wilayani Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu, Kassim Majaliwa aliwabwaga wapinzani wake katika ujumbe wa NEC baada ya kupata ushindi wa kura 578, huku Kalembo Napenya akiambulia kura (254) na Namkumbya Hassan (250).
Aidha, katika nafasi ya uenyekiti wa CCM wilayani hapo, Njinjo Mussa alishinda kwa kupata kura 704 huku wapinzani wake ambao ni Adelfina Joseph (174) na Selemani Mmuya (324).
Katika wilaya ya Lindi Vijijini, Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda alishinda nafasi ya ujumbe wa NEC kwa kupata kura 1,066 huku wapinzani wake ambao ni Mikidadi Alawi wakiambulia kura 277 na Shaibu Buriyani (276) kati ya kura 1,196.
Gefi alisema katika wilaya hiyo nafasi ya mwenyekiti wa CCM wilaya ilienda kwa Mohammed Nyangamara aliyeshinda kwa kupata kura 535 huku wapinzani wake Masudi Chitende (246) na Athumani Hongonyoko (415).
Kwa upande wa wilaya ya Kilwa, nafasi ya uenyekiti wilaya ilinyakuliwa na Yusufu Kopakopa aliyepata kura 873 huku wenzake ambao ni Ally Mngindo akiambulia (452) na Mikidadi Kinogeandaga (271) kati ya kura 1,566 zilizopigwa.
Nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika wilaya hiyo ilichukuliwa na Balozi Ally Mchumo aliyepata kura 1,113 na wakati Njuma Ibrahim alipata kura (56) na Saidi Mkunga (435).
Katibu huyo wa CCM mkoa wa Lindi pia alithibitisha ushindi wa mke wa Rais, Salma Kikwete katika ujumbe wa NEC kwa wilaya ya Lindi Mjini, baada kupita bila kupingwa.
Aidha alisema nafasi ya uenyekiti wa wilaya hiyo ya Lindi, ilichukuliwa na Muhsin Ismail aliyepata kura (476) huku wapinzani wake ambao ni Abdallah Livembe wakiambulia kura 138 na Manyanya Nasibu (38) kati ya kura 655 zilizopigwa wilayani hapo.
Nyalandu apeta Singida Mkutano Mkuu wa uchaguzi CCM wilaya ya Singida vijijini, umemchagua Naibu Waziri wa maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia wilaya hiyo. Nyalandu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini, alipata nafasi hiyo baada ya kukomba kura 897 kati ya jumla ya kura 1,157 zilizopigwa.
Mpinzani wake wa karibu, Dafi Bulali aliambulia kura 131, Manase Sabasaba alipata kura 102 na Juma Mwiru kura 27 tu.
Naye Justin Monko, mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi, Amani Nyekele, Rehema Majii na Aziza Kiduda walichaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa Taifa.
Narumba Banarbas, ambaye alikuwa anatetea nafasi yake ya mwenyekiti wilaya CCM alifanikiwa kufanya hivyo baada ya kupata kura 607 ambapo Mwiru Juma alipata kura 480.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi huo, Moses Matonya, washindi wa nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu wilaya kundi la vijana ni Manase Sabasaba, Jumanne Salum, Daud Elias na Hilda Lazaro Wajumbe wa halmashauri wilaya kupitia kundi la wanawake ni Amina Mweri, Hilda Lazaro, Neema Matiti na Zuena Mohammed wakati nafasi za wajumbe wa halmashauri kuu kundi la wazazi ni Justin Monko, Edward Yaredi, Ilanda na Ramadhani Mangu.
Katika uchaguzi uliofanyika wilayani Ikungi, Mkandarasi mashuhuri wa majengo mkoani hapa, Hassani Tati alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo kwa kishindo.
Tati alichukua nafasi hiyo kwa kupata kura 968 dhidi ya washindani wenzake wawili, Bwaba Mpaki Ibrahimu aliyepata kura 211 na Athuman Magwe aliyepata kura 89. Naye Jonathan Njau ambaye alinyang’anywa nafasi ya ubunge na Tundu Lissu wakati wa Uchaguzi mkuu mwaka 2010, safari hii alichaguliwa kwa kishindo na mkutano huu kuwa mjumbe wa NEC kupitia wilaya hiyo.
Njau alifanikiwa kupata kura 775 na hivyo kuwabwaga vibaya washindani wenza Hamisi Ngila na Mkhotya Moris. Nafasi ya mkutano mkuu taifa waliochaguliwa kuwakilisha wilaya ni pamoja na mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku, Theresia Nkuhi, Mkuu wa wilaya ya Ikungi Manju Msambya, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Celestine Yunde na Samwel Gabriel Dinawi.
Kutoka UVCCM ni Paulo Hema (732) na Reuben Elisha Abraham (671) na UWT ni Amina Omari Munjori (774) na Amina Mdandau (654). Halima Mlacha Dar na Abby Nkungu, Singida

No comments:

Post a Comment