Sunday, October 7, 2012

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA KUMI


■UNAPENDWA NA KUOGOPWA NA WATU WENGI DUNIANI
■UKO HATARINI KUPOTEZA ASILI YAKE KABISA
Na Onesmo Ngowi
Masumbiwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea...
Mchezo huu umegawanyika katika sehemu mbili, nazo ni ngumi za ridhaa ambazo washiriki hucheza kwa kugombania tuzo mbalimbali kama medali au vikombe. Ngumi za ridhaa huchezwa kwa raundi tatu za dakika tatu au raundi tano za dakika mbili kila moja. Mchezo huu hufanyika katika katika ngazi ya klabu, mkoa, taifa, bara, dunia na Olimpic.
Pengine ni katika mashindano ya Olimpic ambapo kila bondia wa ngumi za ridhaa hutaka kuwa bingwa. Aina nyingine ya ngumi au masumbwi ni ngumi za kulipwa ambapo wapiganaji hucheza kwa kugombania mikanda mbalimbali zikiwa ni pamoja na fedha.  Ngumi za kulipwa huchezwa kuanzia raundi nne hadi raundi kumi na mbili za dakika tatu kila moja. Mapmabno ya ubingwa huanzia raundi kumi hadi kumi na mbili
Bondia Jack Jonson (Galveston Giant) wa Marekani kulia bingwa wa ngumi miaka ya 1878
Kama nilivyokwisha sema hapo mwanzo, kumbukumbu nyingi zinaonyesha kwamba historia ya mchezo wa ngumi ilianzia kusini mwa Ulaya wakati wa upinzani wa dola za Kiyunani na Kirumi miaka ya 4000 kabla ya kristu. Wayunani waliamini kuwa mchezo wa ngumi ulichezwa na miungu yao kwa Olympus na hivyo kuufanya kuwa sehemu ya mashindano ya mwanzo ya michezo Olimpic yaliyofanyika Uyunani katika miaka ya 688 kabla ya kristu. Mwanzoni mchezo huu ulikuwa unachezwa kwa kutumia mikono mitupu na baadaye kwa kutumia vifaa vilivyozunushiwa mikononi kwenye sehemu ya kupigia ili kuongeza ukali wa ngumi. 
Warumi walianza kutumia mikanda ya ngozi iliyozungushiwa mikononi  ambapo enzi za dola yao ulikuwa ni mchezo uliopendwa sana na wengi.
John Sulivan, bingwa wa ngumi asiyevaa glovu mikononi
Kuanguka kwa dola ya Kirumi kuliufanya mchezo wa ngumi ukose msisimko na baadaye kutosikika kabisa.
Ngumi zilifufuka tena kwenye karne ya 18 wakai wa dola ya Kiingereza hususan wakati ambapo bondia James Figg alipokuwa bingwa wa uzito wa juu kuanzia mwaka 1719 hadi 1730. Hii iliufanya mchezo wa ngumi kupendwa sana na watu wa kipato cha chini au kwa maana nyingine wafanyakazi wa kima cha chini wakati wa mapinduzi makubwa ya viwanda yaliyotokea huko Ulaya katika karne ya 18. Watu mbalimbali walilazimika kushiriki kwenye mchezo huu kama sehemu ya kipato chao.
Mwaka 1866 mtawala wa Queensbury (Marguees of Queensbury) huko Uingereza alisaidia kutunga sheria mpya zilizotumika kuuendesha mchezo wa ngumi sheria ambazo kwa heshima zilipewa jina lake. Sheria hizi zilipunguza muda uliotumika kwenye raundi za mpambano wa ngumi, na pia ziliweka kikomo kwa mabondia kuangushana chini kama wacheza mieleka. Zilifanya pia matumizi ya gloves kuwa ya lazima. Kabla ya hapo mabondia walikuwa wanatumia mikono mitupu (bare-nuckle) na wengine walivaa vifaa vilivyowawezesha kuumizana vibaya sana.
Pamoja na sheria hizi mpya kupigana kwa kutumia mikono mitupu (bare-knuckle) hakukuisha mara moja hadi mwaka 1892 wakati bondia James J. Corbet alipomshinda bingwa maarufu aliyejulikana kwa kucheza kwa mikono mitupu John L. Sullivan ndipo matumizi ya gloves yalipoanza kutumika katika mapambano yate ya ngumi.
Ngumi hazikuwa na umaarufu huko Amerika hadi miaka ya 1800. Kuanzia miaka hiyo mchezo wa ngumi umekuwa unatawaliwa sana na wamarekani haswa katika mashindano ya Olimpiki ambapo wameweza kutwaa medali 47 za dhahabu kati ya 191. Ngumi zilirudi rasmi katika mashindano ya Olimpic mwaka 1904 wakati yalipofanyika katika mji wa St. Louis, Mo, USA.
            Mmoja wa mabondai wa mwanzo kwenye ngumi za Kulipwa
Mchezo huu huchezwa kwenye ulingo wa mraba wenye vipimo vya futi 18 kwa 18 na ulingo wenyewe huzungushiwa kamba kati ya tatu au nne ili kuwazuia wapiganaji wasitoke nje. Ndani ya ulingo wenyewe kuna kona nne mbili kati ya hizo zikiwa ni nyekundu na bluu na zilizobaki rangi ya njano au nyeupe ikiashiria kuwa ni neutral.
Mabondia wawili wanaocheza husimama kwenye kona hizi nyekundu na  bluu na refarii husimama kwenye kona mmojawapo ya njano. Kila bondia anatakiwa asimame au kukaa kwenye kiti kilichopo kwenye kona yake hadi refarii aashirie mwanzo wa raudi. Kila mwisho wa kila raundi refarii husimama kwenye kona mojawap ya njano kwa muda wa mapunziko. Muda huu kwa kawaida ni dakika moja.
Mabondia wawili wanaocheza ngumi ni lazima walingane uzito. Uzito huu huanzia lightflyweight chini ya kilo 50, flyweight (kilo 50.8); bantamweight (kilo 53.5); featherweight (kilo 57.2); lightweight (kilo 61.2); welterweight (kilo 66.7); middleweight (kilo 72.6); light heavyweight (kilo 79.4); and heavyweight (ambayo haina mwisho). Katika miaka ya karibuni kumeongezeka uzito katikati ya uliotajwa hapo juu kama junior au super.
Kwa kawaida mabondia huvaa gloves za kuchezea mikono yote miwili zenye uzito tofauti kufuatana na uzito wao. Jinsi uzito wa mabondia unavyokwenda juu gloves zenyewe huwa ndogo zaidi. Aidha huvaa kaptula na viatu maalum vya kuchezea. Ndani ya kaptula zao huvaa kifaa maalum cha kuzuia bondia asiumizwe wakati mpinzani wake akimpiga kwa bahati mbaya chini ya mkanda, kifaa hiki huitwa protector. Mabondia wote lazima wavae mipira maalum inayozuia midomo yao isikatike inayojulikana kama gumshield.
HAPA NCHINI TANZANIA kila kukicha wadau wa ngumi wanasoma kwenye magazeti au kusikia kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuhusu migogoro isiyoisha kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa. Migogoro mingi imekuwa inaanzishwa kwa manufaa ya wahusika badala ya malengo yanayodaiwa kulenga. Hii inachangiwa na kuwepo kwa dhana potofu kwamba mchezo wowote unatakiwa uongozwe na wachezaji waliostaafu.
Hata kama kuna ukweli fulani lakini vyama vya michezo kama taasisi nyingine yoyote vinayoongozwa na katiba zinazoainisha barabara wanaohusika katika uongozi wake. Kwa kawaida katiba zinaweka bayana kuwa wahusika wa mchezo huo ndio hao wanaoruhusiwa kuendesha chama. Mara nyingi migogoro kwenye taasisi nyingi hutokea kutokana na sababu ya ufahamu mdogo wa wanachama kuhusu katiba zao.
Kwa mfano wanaohusika kutunga katiba wanaweza kuweka vipengele vya kuwapa nafasi ya kukaa madaraka kirahisi. Mara  nyingi wanaoandika katiba wanachukua nafasi ya uelewa mdogo wa wanachama wa taasisi kujiwekea vifungu hivi.Ndiyo maana ya kuwa na ngazi mbalimbali za kuipitia na kuipitisha katiba.
Ngazi mojawapo muhimu ni mkutano mkuu wa wanachama ambao unaoitwa ili kuipitia na kuipitisha katiba. Katika ngazi hii wanachama wenyewe ndio wenye uwezo wa kuipitisha au kuikataa katiba husika. Linapotokea hili la kuikataa katiba vifungu tata hujadiliwa na kurekebishwa na hatimaye katiba kupitishwa.
Lakini kwa sababu ya uelewa mdogo wa wanachama kuhusu masuala ya katiba wanaweza kutokuwa na uwezo wa kuona mapungufu ya katiba inayoletwa kwao kuipitisha. Matokeo yake wakapitisha katiba mbovu.
Hata kama kasoro hii inatokea kuna ngazi nyingine muhimu zaidi ambayo huipitia na kuiidhinisha katiba yenyewe. Ngazi hii ni ya msajili wa taasisi husika. Umuhimu wa msajili hutokana na uwezo wa kisheria wa maswali ya katiba waliyo nayo. Wao wanayo format inayotakiwa kufuatwa ili katiba za taasisi zilizo chini yao zipitiwe.
Msajili ni ofisi ya Serikali anayehusika kuipitia katiba za taasisi kwa makini ili zisije kuwa na mapungufu yanayoweza kuchochea migogoro. Baada ya kuiridhia katiba msajili hutoa kibali cha kuikubali na kuirudisha kwenye taasisi ili itumike kama dira ya taasisi hiyo.
Kwa hiyo taasisi iliyokwisha kuwa na katiba iliyoridhiwa na msajili ni taasisi  iliyokamilika na inayomilikiwa na wanachama walioainishwa kwenye katiba yenyewe. Sifa za wanachama zinatajwa waziwazi kwenye katiba. Na hii inaipa katiba nguvu za kipekee kutumika kukiendesha chama/taasisi kufuatana na taratibu, kanuni na sheria zilizotajwa kwenye katiba husika.
Pamoja na mambo haya kujulikana, lakini ni wanachama au wadau wachache wanaofuata katiba za taasisi husika. Wadau wengi na baadhi ya wanachama hawajui taratibu zinazotakiwa ili kuendelesha taasisi kwa mafanikio. Ama wanasukumwa na matakwa binafsi au wanatumiwa na wachache walio na kiu cha kufaidika na migogoro.
Taasisi ya michezo kama zilivyo taasisi nyingine zote huendeshwa kwa kufuata katiba. Ni dhana potofu kufikiria kwa kuwa mtu alikuwa mchezaji wa mchezo wa ngumi basi ana haki ya kukiendesha chama. Mfano mmoja ni jinsi vyama vya mchezo wa ngumi vya kimataifa kama IBF,WBA na WBC vinayoongozwa.
Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chama cha Ngumi Cha Marekani (IBF/USBA) liliwahi kuongozwa na mama Marian Muhammad mke wa zamani wa promota Murag Muhammad ambaye hajawahi kuvaa gloves maishani mwake. Mama Muhammad ni mtaalam wa uongozi wa mchezo wa ngumi. Akiwa pamoja na Bob Lee sr., Hiawatha Knight na wengine mwaka 1983 walianzisha USBA na baadaye USBA-1 na leo hii IBF/USBA.
Uamuzi huu ulifikiwa baada ya Wamarekani wengi ambao walikuwa kwenye uongozi wa WBA kukosa imani jinsi Chama hiki  kilivyokuwa kinaongozwa. Kabla ya kuanzisha USBA wote watatu walikuwa kwenye safu ya uongozi wa WBA.
Kuanzishwa kwa USBA kulikuwa ni kama ukombozi kwa mabondia wengi wa Marekani ambao walihisi kuwa wenzao wa Amerika ya kusini waikuwa wanapewa nafasi nzuri za viwango na ubingwa.  Hivyo shirikisho la ngumi la kimataifa na chama cha ngumi cha  Marekani IBF/USBA vimeshatoa mabingwa wengi wa dunia yakianzia na Larry Holmes hadi kina Mike Tyson.
Sifa za kuwa kiongozi wa IBF/USBA sio kuwa bondia mstaafu. Kama nilivyokwishaeleza kuwa rais wake ni mama Marian Muhammad akiongoza bodi ya wakurugenzi ya watu 12 wanaotakiwa kustaafu kila baada ya miaka 3.
Katika uongozi wa kila siku anasaidiwa na watu wafuatao; mwenyekiti wa viwango Daryl J. Peoples, mwenyekiti wa kamati ya ubingwa Lidsey Tucker jr., mwanasheria Linda Torres, rais wa bara la Ulaya Benedetto Montella, rais wa bara la Pasific na Ocenia  Ray Wheatler na rais wa bara la Africa Onesmo Ngowi. Ni Onesmo Ngowi pekee aliyekwisha kucheza ngumi lakini uteuzi wake kamwe hautategemea kuwa bondia wa mstaafu.
Mashirikisho mengine ya ngumi kama WBC kinaongozwa na Jose Suleiman  kutika Mexico na WBA kinaongozwa na  Dr. Gilberto Mendoza kutoka Venezuella. Hata mmoja kati yao hajawahi kucheza ngumi. Ukiangalia utitiri wa mashirikisho mengine ya ngumi kama WBO,WBF,IBO,IBU na mengine yanaongozwa na watu ambao nao hawajawahi kucheza ngumi maishani mwao. Lakini vyama vyote hivi vina mafanikio makubwa katika utendaji wao wa kazi. Iaendelea...
Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com

No comments:

Post a Comment