Friday, April 5, 2013

VIGEZO VYA UTANASHATI, FIGA BOMBA NI MUHIMU ZAIDI?


NIPO hapa kwa ajili yako rafiki yangu. Karibu tubadilishane mawazo kidogo kuhusu maisha yetu ya uhusiano. Naamini somo linasomeka sawia hapo juu. Kazi yako ni kufungua ubongo wako, uweze kuongeza maarifa.
Katika harakati za kusaka wenzi, vijana wengi wamekuwa wakibabaika juu ya sifa za mwenzi ambaye anaweza kuwa sahihi katika maisha yake. Hili limekuwa tatizo sugu hasa kwa vijana wengi!
Lakini vijana wa sasa huhadaika zaidi na mvuto wa sura na maumbile ya mtu wakifanya kama kipimo kikuu cha anayefaa kuwa mwenzi wa maisha, jambo ambalo ni makosa makubwa sana.
Kudanganyika na uzuri wa nje pekee siyo kati ya sifa muhimu zaidi za kumfanya awe na sifa za kuwa mwenzi wako wa maisha. Zamani, wazee wetu walikuwa wanatizama kwanza heshima na uchapakazi kama vipimo vya awali vya kumpa sifa mwanamke kuolewa. Siku hizi ni kinyume chake.
Lakini inashauriwa kuwa makini sana na uchaguzi wako wa mke/mume kwani kufanya maamuzi yasiyo sahihi ni sawa na kujirudisha mwenyewe nyuma. Kuwa na msimamo, fanya uchaguzi ulio sahihi, ambao hautakufanya baadaye ujutie!
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kuhakikisha unakifikiria ni juu ya mapenzi yako kwake! Sema na moyo wako ukupe ukweli juu ya hilo, usikurupukie mapenzi, usije ukamuona msichana siku moja amevaa suruali inambana kiasi cha kuonyesha umbile lake halafu ukamtamani ukadhani unampenda, utakuwa unapotoka!
Mapenzi siyo kitu cha mchezo, huanza moyoni jiridhishe kwanza ndipo ukubali kumwingiza katika moyo wako. Kumbuka kuwa unapoamua kufunga ndoa na mtu ni ahadi ambayo mmeahidiana mbinguni na duniani, ni ahadi ambayo inapaswa kutenganishwa na kifo tu, siyo vinginevyo! Kamwe usifanye majaribio katika mapenzi, mapenzi hayajaribiwi!
Kitu cha pili ambacho unatakiwa kukiangalia ni kuhusu mapenzi yake ya kweli kwako. Wataalam wa Mambo ya Mapenzi wanasema, ingawa ni vizuri kuishi na mtu unayempenda lakini pia ni lazima awe anakupenda! Siyo vigumu sana kumfahamu mwenzi anayekupenda, lakini pia inawezekana ukaona anakupenda kumbe ni danganya toto!
Kimsingi katika hili ni lazima utumie akili yako yote uweze kutambua hilo. Katika makala zangu zilizopita nilianisha sifa za mpenzi mwenye mapenzi ya dhati, lakini kwa kuongezea ni kwamba, anayekupenda huwa mvumilivu, anayekusikiliza pia mwenye kuwajali ndugu, marafiki na jamaa zako, anayekuheshimu na kutambua thamani yako!
Anayetakiwa kuwa mwenzi wako wa maisha lazima awe makini na mwenye akili za kimaisha. Siyo lazima awe na elimu ya darasani, haijalishi ni mwanamke aliyekulia vijijini au mjini, lakini hapa tunaangalia uwezo wake wa kufikiri. Hata hivyo,                inategemea wewe umepanga kuishi na mwanamke wa aina gani, lakini mwanamke ninayemzungumzia hapa ni yule mwenye uwezo wa kutosha wa kufikiri na kupambanua mambo. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na  All About Love vilivyopo mitaani.

No comments:

Post a Comment