Friday, March 7, 2014

Usijidanganye, ndoa siyo majaribio!


NIPO hapa kwa ajili yenu marafiki zangu wapendwa, tujifunze pamoja namna ya kuendelea kuwa bora katika uhusiano na wenzi wetu. Nafurahi kuona wengi wamebadilishwa kabisa na makala ninazoziandika.
Ndugu zangu, vijana wengi (hasa wasichana) hutamani sana kuingia kwenye ndoa. Ni kweli, ndoa ina raha yake lakini pia ina changamoto nyingi sana. Kwa maneno mengine, ni rahisi zaidi kusema kuwa, hakuna kufanya majaribio kwenye ndoa – inahitaji kujipanga ili ukiingia usifikirie kujitoa kwenye taasisi hiyo.
Ukifanya makosa leo mara moja tu, unakuwa umeyagharimu maisha yako yote. Najua vijana wengi wanapata wakati mgumu sana unapofikia wakati ambao wanadhani umri wao unawapasa kuingia kwenye ndoa bila mafanikio.
Zipo dhana nyingine ambazo si sahihi. Msichana akiwa na zaidi ya miaka 25, anajiona ana nuksi na amekosa bahati ya kupata mume wake wa ndoa. Eti ndoa ni bahati! Si kweli. Si suala la bahati...huja kwa wakati unaostahili!
MAMBO MUHIMU YA KUJUA
Kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa na mwenzi uliyempenda, yapo mambo ya msingi sana ambayo ni vyema kama ungeyapa kipaumbele kichwani mwako.
Huna sababu ya kuingia kwenye ndoa kama majibu ya maswali yako uliyojiuliza si mazuri. Yana viashirio vibaya. Lazima kwanza majibu yako yawe mazuri yenye kukupa matumaini mapya katika maisha yako ya ndoa.
Jiulize, kabla ya kukutana na huyo ambaye unatarajia kuingia naye kwenye ndoa, awali uliota kuwa na nani? Lazima kichwani mwako ulikuwa na mtu uliyekuwa unawaza kuwa naye.
Zipo sifa za kawaida ambazo mtu anaweza kuvutiwa nazo kabla ya kukutana na mtu ambaye anadhani anaweza kuwa wake kwenye ndoa. Itakuwa vichekesho mwanaume kukubali kuingia kwenye ndoa na mwanamke mwembamba sana, wakati kichwani mwake alikuwa akivutiwa zaidi na wanawake wenye maumbo makubwa!
Ndugu zangu, ingawa wengi wanakwepa ukweli huu lakini ni kweli kabisa kuwa, kila mmoja huwa na chaguo lake kichwani kabla ya kukutana na mhusika wake. Uliwaza nini kabla? Kuwa na mwanaume mweusi au mweupe?
Acha kubahatisha, hakikisha unayekuwa naye ni yule ambaye ulitamani kabla ya kukutana naye. Ukilazimisha kuwa na mtu ambaye unajua wazi kwamba moyo wako haujaridhika ni tatizo kubwa sana hapo baadaye.
Siri ya pendo la dhati lipo ndani ya moyo wa mhusika. Lazima moyo wako ukiri kwamba aliye mbele yako unavutiwa naye kwa kila kitu. Hutakiwi kuwa na ukakasi wowote moyoni mwako. Kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa, lazima moyo wako uridhie na ukupe kibali rasmi kwamba, sasa umeridhia kuingia katika muunganikiko huo.
VIPI KASORO ZAKE?
Hakuna aliyekamilika chini ya jua, lakini kuna wengine kasoro zao zinavuka mipaka. Ni kweli ni vyema kujifunza kusamehe lakini kuna maeneo mengine ni magumu zaidi kuweza kusameheka kwa urahisi.
Mfano umemfumania mpenzi wako zaidi ya mara tatu, hutakiwi kuendelea kung’ang’ania kwamba unampenda na unataka kuingia naye kwenye ndoa.
Uchumba tu umemfumania mara tatu, mkioana si ndiyo ataingia na mpenzi wake hadi chumbani kabisa?
Hakuna sababu ya kukimbilia ndoa marafiki zangu, lakini jambo la msingi ni kujua unakwenda kwenye ndoa na nani.
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments:

Post a Comment